YOWERI MUSEVENI ATANGAZWA MSHINDI UCHAGUZI WA URAIS UGANDA



Yoweri Museveni ametangazwa kuwa rais mteule Uganda baada ya kupata ushindi wa kura asilimia 58.64.

Tume ya Uchaguzi Uganda (EC) imemtangaza Yoweri Kaguta Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika Alhamisi tarehe 14 Januari 2021.

Kwa mujibu wa EC Bw Museveni amepata kura 5,851,037 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote zilizopigwa.

Mpinzani mkuu wa Museveni, mwanamuziki Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine, ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 3,475,398 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.

Bobi Wine hata hivyo alitangaza kutokukubaliana na matokeo hapo jana wakati tume ya EC ilipokuwa ikiendelea kutangaza matokeo.



Idadi kamili ya watu waliopiga kura ni 9,978,093 ikiwa ni sawa na asilimia 57.22 tu ya idadi ya watu waliojiandikisha kwenye daftari la wapiga kura.

Hii inamaana kuwa zaidi ya asilimia 40 ya waliojiandikisha hawakujitokeza kupiga kura.

Rais Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 35 akiwa atakuwa anaingia kuongoza kwa muhula wa sita.

Bwana Museveni mwenye miaka 76-anasema kuwa amelifanya taifa hilo kuwa na maendeleo wakati Bobi Wine, ambaye ana miaka 38- jina lake alisi likiwa Robert Kyagulanyi, anasema anawakilisha vijana ambapo Uganda likiwa ni taifa ambalo lina vijana wengi zaidi duniani.

Ijumaa, wakati matokeo yakianza kutangazwa bwana Wine alisema askari walikuwa wameizingira nyumba yake.

Lakini msemaji wa serikali alimshutumu kwa kuweka taharuki isiyo na ukweli ili kupata huruma ya watu.

 CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments