WAZIRI JAFFO ATAKA VIONGOZI NA WASIMAMIZI WA MRADI WA UJENZI WA MAJENGO YA UVINZA KUKAMATWA NA KUWEKWA NDANI


Jengo la Utawala la halmashauri ya wilaya Uvinza ambalo ujenzi wake umekwama
Jengo la nyumba ya Mkuu wa wilaya Uvinza ambalo limekwama tangu mwaka 2013 licha ya watekelezaji wa mradi wakala wa majengo (TBA) kupokea milioni 500 kwa ajili ya ujenzi huo
**

Na Editha Karlo,Uvinza

WAZIRI wa Tawala za mikoa na serikali za mitaa Suleiman Jaffo ameamuru kukamatwa na  kuwekwa ndani kwa viongozi na wasimamizi wa miradi wa wakala wa majengo nchini (TBA) mkoa Kigoma kwa kushindwa kukamilisha miradi ya ujenzi waliyopewa wakati walichukua kiasi kikubwa cha pesa.

Jaffo ameyasema hayo leo kwenye ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Kigoma 

Akiwa kwenye ziara ya kukagua majengo ya Utawala ya viongozi na watumishi walio chini ya wizara hiyo Wilayani Uvinza alikerwa na taarifa ya ujenzi wa majengo hayo.

Akiwa wilayani Uvinza Waziri  Jaffo alieleza kukerwa   na taarifa ya  TBA kupewa kiasi Cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Wilaya ya Uvinza miaka mitano iliyopita ambapo hadi Sasa nyumba hiyo imefikia usawa wa msingi.

Pamoja na hiyo Waziri Jaffo alionyesha kukerwa kutokana na kukwama jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya Uvinza ambapo kiasi Cha shilingi milioni 900 kimetolewa lakini mradi umekwama kwa miaka zaidi ya mitatu na kwa sasa ujenzi upo usawa wa madirisha.

Akitoa taarifa kwa Waziri Jaffo Meneja wa miradi ya ujenzi katika ofisi ya Mkuu wa mkoa Kigoma, Masawika Kachenje alisema kuwa miradi hiyo ilianza mwaka 2013 na ilipaswa kukamilika mwaka 2018 na waliomba pesa kwenye miradi hiyo kama malipo ya awali.

Kachenje alisema kuwa pesa kwenye miradi hiyo zimeingizwa kwenye akaunti ya TBA makao makuu lakini taarifa zinaonyesha kuwa pesa hizo hazipelekwi kwenye miradi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya Uvinza,Mwanamvua Mrindoko alimweleza Waziri Jaffo kuwa analazimika kuishi kwenye nyumba za kontena zilizoachwa na mradi wa ujenzi wa barabara za kiwango cha lami wa Kidahwe Hadi Uvinza kutokana na kukwama kwa ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa wilaya.

Mrindoko alisema kuwa wamefanya jitihada kuhakikisha TBA wanarejesha fedha lakini hakuna jitihada iliyofanyika.

Kutokana na hali hiyo Waziri Jaffo ameagiza kuorodheshwa kwa miradi yote iliyokwama kwa mkoa wa Kigoma ambayo ilikuwa inatekelezwa na TBA, kueleza thamani ya kazi iliyofanyika na kiasi Cha pesa kilichoelekwa na taarifa hiyo iwasilishwe ofisini kwake aweze kuifanyia kazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post