BARAZA LA MCHELE TANZANIA (RCT) LAWAFUNDA WASINDIKAJI WA ZAO LA MPUNGA 100 KANDA YA ZIWA KULETA USHINDANI SOKO LA KIMATAIFA


Mkurugenzi mkuu  baraza la Mchele Tanzania (RCT) Winnie Bashagi akielezea kuhusu usindikaji wa zao la mpunga katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo maalum ya kuwajengea uwezo wa kusindika mchele yanayoendelea mjini Kahama.
Katibu tawala wa wilaya ya Kahama Timothy Ndanya akizungumza na baadhi ya wasindikaji hawapo (pichani) kutoka mikoa ya kanda ya ziwa ambao wanaendelea na mafunzo maalumu ya kusindika mchele katika viwango vya kimataifa.
Mtafiti kutoka taasisi ya Utafiti nchini(REPOA) Steven Mombela akizungumza na wasindikaji wa zao la mpunga katika mafunzo maalumu yanayoendelea kufanyika wilayani kahama na kuhudhuriwa na washiriki 100 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao ni wasindikaji wa zao la mpunga wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi hayupo pichani ambaye ni katibu tawala wa wilaya ya Kahama Timothy Ndanya.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo ambao ni wasindikaji wa zao la mpunga wakimsikiliza kwa makini mgeni rasmi hayupo pichani ambaye ni katibu tawala wa wilaya ya kahama Timothy Ndanya.
**
Na Salvatory Ntandu - Kahama

Baraza la mchele Tanzania(RCT) kwa kushirikiana na taasisi ya utafiti Tanzania (REPOA) wanaendesha mafunzo kwa wasindikaji wa mpunga 100 kutoka mikoa ya Geita,Shinyanga, na Tabora ili kuwajengea uwezo wa kusindika bidhaa hiyo kwa viwango vya kimataifa.

Hayo yamebainishwa jana na Mkurugenzi mkuu wa baraza hilo, Winnie Bashagi katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo ya siku tatu kwa wasindikaji wa zao la mpunga kutoka mikoa ya kanda ya ziwa  na kusema  kuwa mchele wa Tanzania unakosa soko kimataifa kutokana na kutofungashwa kwa viwango vya kimataifa.

Alisema  zaidi ya asilimia 80 ya mchele unaozalishwa na wakulima wadogo  katika wilaya zaidi ya  64  hapa nchini unakosa sifa katika masoko ya kikanda ya jumuia ya afrika mashariki (EAC) na (SADC) kutokana kutosindikwa kwa viwango vinavyotakiwa licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa.

“RCT na REPOA tulifanya utafiti katika wilaya zinazolima zao hili tulibaini kukosekana kwa elimu ya usindikaji,wasindikaji wengi wanachanganya madaraja,usafi,usimamizi usiridhishwa wa magahala ya kuhifadhia mpunga,matumizi yasiyosahihi ya pembejeo kwa wakulima wakati wa kuandaa mashamba,”alisema Bashagi.

Awali akifungua mafunzo hayo ya siku tatu Katibu tawala wa wilaya ya Kahama Timoth Ndanya kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack aliwataka (RCT) kufungua ofisi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kuwajengea uwezo wakulima na wasindikaji katika kuongeza thamani mazao yao.

“Kahama tunazalisha mpunga wa kutosha hakikisheni mnawajengea uwezo wasindikaji na wakulima wa zao hili la biashara ili kuwainua kiuchumi hakuna sababu ya wao kuendelea kukosa masoko ilihali wanamchele safi ambao unahitaji kupangwa katika madaraja yanayotakiwa kimataifa,”alisema Ndanya.

Naye Steven Mombela mtafiti kutoka (REPOA) alisema wao kwa kushirikiana na baraza la mchele wanatekeleza mradi huo ujulikanao kama Tradecom II kwa ufadhili wa jumuiya ya ulaya (EU) na waliandaa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo ili waweze kuzalisha mchele wenye viwango vinavyokidhi ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.

“Mradi huu ni wa miaka miwili ulianza mwaka 2020 na unatarajiwa kukamilika mwaka huu,na tukimaliza kwa kanda hii tutaelekea katika kanda nyingine inayojumuisha wasindikaji kutoka mikoa ya Morogoro,Njombe,Iringa na Mbeya,”alisema Mombela.

Asha Hassan Msangi ni mmoja wa  wasindikaji wa zao mpunga kutoka Kahama ameiomba  Serikali kuboresha mazingira ya biashara ya mchele ikiwa ni pamoja na kufungua masoko ya mchele na kuwazuia wafanyabiashara wa nje kununua mpunga kwa wakulima.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments