MZEE ABDUL : "MSINIITE TENA BABA DIAMOND, AKITUMIA JINA LANGU NAMSHTAKI....NI JEURI YA PESA, ANAJIONA HATOKUFA"


IKIWA ni saa chache baada ya mama mzazi wa msanii maarufu wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz, Sanura Kassim maarufu Mama Dangote, kuanika kuwa Mzee Abdul Juma ambaye wengi wanamjua kama baba mzazi wa Diamond, si baba Mzazi wa Diamond kwani wakati wanaingia kwenye mahusiano, tayari mama huyo alikuwa na ujauzito wa mwanamuziki huyo, basi mzee Abdul naye amejibu mapigo.

“Sasa hivi inabidi msiniite Baba Diamond, niiteni Mzee Abdul peke yake, kama alivyoongea mama na mimi najibu kwa ufupi, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwa Baba mlezi, nimepata thawabu hata kama ni ndogo.

“Kwa aliyozungumza najisikia faraja moyoni mwangu kwa sababu nilikuwa najiuliza, kwa nini nikihitaji kitu nakosa, halafu wengine wanapata. Kumbe walikuwa wamekaa na mtoto wake wamepanga mambo yao na leo napata jibu kamili kwamba mimi sio baba mzazi ni baba mlezi.

“Kwa hiyo atakuwa Diamond Platnumz na siyo Naseeb Abdul, akitumia jina langu nitamshitaki, lakini upande wa Queen Darleen kama yeye atakuwa tayari kubaki na mimi kama baba yake, nipo tayari, Diamond tumeachana asitumie tena jina langu, nitabaki kuwa baba mlezi.

“Leo Watanzania wamejua kwa nini nilikuwa sipati misaada kwa sababu siyo mhusika. Lakini alichofeli huyo mama ni jambo moja tu, mimi nimeishi naye tangu mwanzo, akawa mjamzito, nikalea mpaka nampeleka hospitali anakwenda kujifungua, nimelea mtoto mpaka tukaja kugombana akiwa form one, lakini leo ametoa kauli kama hizo inaonekana walikaa wakapanga na mtoto wake wafanye hivyo.

“Mama Diamond hakuwa na mahusiano mengine, kimsingi mimba ya kwanza tulitoa, mpaka nikauza mkanda wangu wa deki ili tukatoe mimba ile. Baadaye tukafanya tena ndipo akapata ujauzito wa Diamond. Kumbe nilikuwa napigwa picha za kudharirishwa? Na mimi nazungumza kwamba Diamond Platnumz siyo mwanangu, sihusiki naye na sipo kwenye familia yao.

“Mtoto hagombaniwi, hata mpaka wa nyumba haugombaniwi, kama sio riziki yako achana nacho, najua kama asingekuwa na pesa yasingetokea haya, pengine kwa sababu anajiona hatokufa, wamenivunjia adabu, kama ni mambo ya kifamilia wangeniita tukayamaliza kumbe ndiyo maana nilikuwa nababaishwa.

“Diamond alizaliwa Hospitali ya Amana, nilihusika mwanzo mpaka mwisho, malezi na kila kitu lakini hii ni kiburi tu cha pesa, bahati nzuri Diamond hajawahi kunisaidia chochote, nina maisha yangu napata kidogo kinanitosha. Wakamwonyeshe kaburi la baba yake basi, kama atamfanya Queen Darleen ni mfanyazi wake sawa tu,” amesema Mzee Abdul.

Januari 15,2021 Mama Dangote alifunguka kupitia kipindi cha MashamSham, kinachoruka kupitia Wasafi FM baada ya kupigiwa simu LIVE kufuatia mahojiano ya Ricardo Momo ambaye ameelezea kuwa ni kaka yake na Diamond kwani wanashea baba mmoja ambaye anaitwa Salum Iddy Nyange (marehemu kwa sasa).

Sanura Kassim maarufu mama Dangote ambaye ni mama mzazi wa msanii wa Tanzania, Diamond Platnumz amesema baba halisi wa mwanaye ni Salum Iddi Nyange na si Abdul Juma ambaye kwa miaka mingi amekuwa akifahamika kama baba wa mkali huyo wa Bongofleva.

Katika majibu yake, mama Dangote amesema Ricardo na Diamond ni ndugu na baba yao ni Nyange ambaye kwa sasa ni marehemu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post