MWAKALINGA AFURAHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA NCC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga akizungumza wakati akifungua Kikao cha Tatu cha Baraza la Wafanyakazi wa NCC jijini Dar es salaam. 
Mtendaji Mkuu wa Baraza la Wafanyakazi NCC, Dkt. Matiko Samson Mturi akizungumza kwenye Kikao cha Tatu cha Baraza la Wafanyakazi wa NCC lilichofanyika jijini Dar es salaam 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga akifurahia jambo na menejimenti ya Baraza la Wafanyakazi la NCC. 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa NCC jijini Dar es Salaam.

**************************************

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Arch. Elius Mwakalinga amewataka Menejimenti na Watumishi wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kutangaza kazi wanazozifanya ili zieleweke kwa jamii na kuongeza wigo mpana wa kuwahudumia wananchi.

Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa Kikao cha Tatu cha Baraza la Wafanyakazi wa NCC jijini Dar, Arch. Mwakalinga amesema huu ni wakati wa Baraza hilo kushirikiana na taasisi nyingine katika sekta ya ujenzi ili kuboresha huduma za ujenzi na kufanya gharama za ujenzi nchini kuwa za bei nafuu.

"Hakikisheni gharama za ujenzi nchini zinakuwa nafuu na zinazotekelezeka ili kuvutia watu kuwekeza katika ujenzi kwa kuwaelimisha fursa zilizopo na kutatua migogoro ya ujenzi kwa wakati,” amesema Arch. Mwakalinga.

Aidha amemtaka Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Matiko Samson Mturi kuhakikisha watumishi waliopo katika baraza hilo wanakuwa na elimu, ujuzi na umahiri ili tafiti zinazofanywa ziweze kuwa na tija kwa taifa kwa muda mrefu.

“..Hakikisheni kuwa hamuwi wanyonge kwa kuwaendeleza kitaaluma watumishi wenu, kutangaza kazi kubwa mnazozifanya ili jamii izifahamu na kunufaika nazo na kufanya tafiti zinazoleta unafuu wa maisha kwa jamii ikiwemo kutayarisha wataalam wa ushuluhishi wa masuala ya ujenzi,” amesisitiza Katibu Mkuu, Arch. Mwakalinga.

Naye Mtendaji Mkuu wa NCC, Dkt. Matiko Mturi amesema kati ya mwaka 2018 hadi 2023 baraza limejipanga kuhakikisha migogoro mingi ya ujenzi inatatuliwa huku wadau wa ujenzi wakielimishwa ili kuepuka migogoro.

“Tumejipanga kuhakikisha tunaboresha idara ya utafiti ili masuala mengi yanayoamuliwa na baraza hilo yawe ni matokeo ya tafiti za kina, ambayo yatakuwa hayajirudii mara kwa mara,” amesema Dkt. Mturi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments