KAMANDA AJINYONGA AKIACHA UJUMBE ".....MKE WANGU ANANIFANYIA MAMBO YA KISHIRIKINA"

Picha haihusiani na habari hii hapa chini

Na Mary Clemence - Katavi
 Samweli Mbingilwa (54) almaarufu kama Kamanda amejinyonga hadi kufa akiacha ujumbe kuwa ‘mke wangu si mwaminifu katika ndoa na ananifanyia mambo ya kishirikina.’

Mwili wa Mbingilwa aliyekuwa mkazi wa Tambukareli mjini Mpanda ulikutwa kwenye kiti huku kamba ya chandarua aliyojifunga juu na kujining’iniza ikiwa kimekatika.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Katavi, Abdi Issangu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema “ni tukio la kweli na mwanaume huyo ameacha ujumbe unaosema, ‘mke wangu siyo mwaminifu katika ndoa na ananifanyia mambo ya kishirikina.”

Mke wa marehemu, Maria Nswima alisema siku kadhaa kabla ya kujiua, mumewe alichoma moto nguo zake huku mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Tambukareli, Selestino Shauritanga akisema Mbingilwa aliwahi kunywa dawa akitaka kujiua.

Akieleza ilivyokuwa, Maria alisema Novemba 25 mwaka huu mumewe alikwenda kilabuni lakini kesho yake kuliibuka ugomvi kati yao na akamtishia maisha.

“Nilimpisha nyumbani ila saa mbili usiku nikarudi akaniambia leo ni siku yako ya mwisho, nikamuuliza kivipi akajibu ya mwisho kuishi. Kuona hivyo niliamua kwenda kwa mwenyekiti lakini sikumkuta...baada ya kurudi nyumbani nikakuta amechoma nguo zangu zote moto na kukatakata masufuria pamoja na kupasua mabakuli yote.”

Kutokana na hali hiyo, alisema “nilienda kituo cha polisi nikaeleza na kupewa wito niliompelekea balozi akampa lakini watoto wakaniambia ameichana, hii hapa. Nikavichukua hivyo vipande na kuvipeleka kwa mwenyekiti akaniambia rudi tena polisi, nikarudi...tangu siku hiyo niliamua kuishi kwa shangazi yangu,” alisema Maria.

Alisema Desemba 5 saa 11 jioni mtoto wake alikwenda kumpa taarifa kuwa baba yao amejinyonga chumbani kwake.

“Baada ya kufika nilikuta ametumia chandarua ambacho kilikuwa imekatika na yeye alikuwa amekaa kwenye kiti akiwa amefariki tayari. Ilikuwa kawaida yake kwenda kunywa pombe akirudi lazima kelele ziwepo lakini baadaye zinaisha,” alisema Maria.

Licha ya uvumilivu aliounyesha kwa miaka amingi waliyoishi pamoja, Maria alisema “awamu hii alizidisha, nikaamua kuondoka. Nimezaa naye watoto saba, naumia kwakuwa nilimzoea. Sikuwahi kufikiria kama anaweza kujinyonga,” alisema.


Soma Habari Hii kwa KINA <<HAPA>>


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post