BABU WA MIAKA 75 AKAMATWA NA SILAHA KAHAMA


Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga Kamishina Msaidizi wa Polisi Debora Magiligimba akionesha Silaha zilizokamatwa na kwa Masanja Maziku Mkazi wa Kahama jana,(Picha na Salvatory Ntandu).

Na Salvatory Ntandu - Kahama

Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia Masanja Maziku Bugolole (75) Mkazi wa Kijiji cha Gula Wilayani Kahama mkoani Shinyanga kwa tuhuma ya kumiliki silaha nne aina ya Shotgun,mitutu sita ya Shotgun na Risasi 36 alizokuwa anazimiliki kinyume cha sheria.

Akizungumza na Waandishi wa habari jana Wilayani Kahama, Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Debora Magiligimba alisema kuwa Masanja alikamatwa Disemba 17 mwaka huu majira ya usiku nyumbani kwake kufuatia msako maalumu unaoendeshwa na jeshi hilo kwa lengo la kuwakamata wahalifu mbalimbali.

Alisema kuwa Silaha zilizokamatwa zimebainika kufutika namba zake za uhakiki na zingine zina namba lakini hazijasajiliwa kama sheria za umiliki wa silaha inavyoelekeza sambamba na kutokuwa na kibali cha kumiliki risasi 36 ambazo alikamatwa nazo.

“Silaha mmoja imebainika kuwa na uhakiki wa namba TZCAR 34951lakini usajili  wake umefutika, silaha tatu hazina namba za uhakiki lakini zina namba za usajili ambazo ni Silaha namba D 172321,14999 na 24162,”alisema Magiligimba.

Magiligimba alisema kuwa baada ya upelelezi wa ukikamilika Masanja atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Sambamba na hilo Kamanda Magiligimba alifafanua kuwa katika msako huo pia Jeshi hilo liliweza kuokota silaha mmoja aina ya Gobole katika kijiji cha Mpera wilayani humo ikiwa imetelekezwa kichakani na kuwataka wakazi wa mkoa wa shinyanga kutoa taarifa za watu wanaomiliki silaha kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga Kamishina Msaidizi wa Polisi Debora Magiligimba akionesha Silaha zilizokamatwa na kwa Masanja Maziku Mkazi wa Kahama jana,(Picha na Salvatory Ntandu).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments