Desemba 23, siku mbili kabla ya Sikukuu ya Krismasi, wanaume jijini Dar es salaa walialikwa katika sherehe ya kuburudika na wanawake wawatakao lakini Jeshi la Polisi limeifuta sherehe hiyo na kuwatia mbaroni waandaaji wake.
Ni sherehe ya ufuska iliyopangwa kufanyika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es salaam, ambayo mhudhuriaji alitakiwa kununua kadi itakayomuwezesha kuingia katika nyumba maalum na humo angekutana na wanawake wa kustarehe nao.
Kwa utaratibu uliowekwa, kulikuwa na kadi ya Sh150,000 ambayo mwanaume angepata mwanamke mmoja na ya Sh300,000 inayompa fursa ya kujipatia wanawake wawili wa kufanya nao uzinzi.
Maandalizi ya sherehe hiyo yalipangwa na kutangazwa katika mitandao ya kijamii lakini Jeshi la Polisi Wilaya ya Kinondoni lilibaini jambo hilo na kuwakamata watano, akiwamo mwandaaji wa sherehe hiyo.
Video mbalimbali zilizosambaa mtandaoni zina sauti ya mtu anayefafanua kuhusu upatikanaji wa kadi hizo, akisisitiza kuwa siku hiyo mambo yatakuwa mazuri na kuwataka wateja kuwahi kuzinunua.
Wakati sauti hiyo ya kike ikisikika kueleza hayo, katika video ilikuwamo namba ya simu kwa watakaotaka kushiriki huduma hiyo ambayo hata gazeti la Mwananchi lilipojaribu kuipiga haikupatikana na wakati likiendelea na uchunguzi, polisi walibainisha kuwakamata watu hao huku jeshi likiendelea kuusaka mtandao mzima unaojihusisha na ufuska huo.
“Hizi ndio tiketi zetu... hii ni ya Sh300,000 unapata wanawake wawili wa kufanya nao mapenzi na ya Sh100,000 unapata mwanamke mmoja wa kufanya naye mapenzi. Kwenye hii tiketi utapata chumba, utaogelea na shoo yangu ya (anaitaja), wote mnakaribishwa Mbezi Beach private house,” anaeleza mwanamke huyo kwenye video inayosambaa mtandaoni.
Kamanda wa polisi, Ramadhani Kingai alisema watuhumiwa hao walikamatwa juzi usiku na bado wanaendelea kuwatafuta wengine waliosambaza video hizo.
CHANZO MWANANCHI