RIDHIWANI KIKWETE : SHIDA YA MAJI KIBINDU KUWA HISTORIA

Shida ya Maji kwenye Vijiji na Vitongoji vya Kata ya Kibindu, Jimbo la Chalinze inatarajiwa kuwa historia kutokana na utekelezaji wa miradi ya Maji ya yenye thamani ya zaidi ya Bilioni 1.6.

Awali Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete akiongea mbele ya Wananchi wa Kijiji cha Kwamduma, amewahakikishia Wananchi wa Kata ya Kibindu kuwa, shida ya maji inaenda kuwa historia kwani tayari shughuli za utendaji zinaendelea.

Mbunge alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano kwa hatua zinazochukuliwa kupata ufumbuzi wa shida ya Maji katika kata hiyo na Jimbo zima la Chalinze.

"Serikali imejidhatiti kuhakikisha maji yanawafikia wananchi wa Kibindu. Niwahakikishie kuwa miradi hii itakamilika kwa wakati na mapema ili wananchi wapate maji safi na salama" alisema Ridhiwani Kikwete.

Pia alieza kuwa, akiwa kama Mbunge amefanya jitihada mbalimbali ikiwemo kuchimbwa kwa visima zaidi ya vinne katika vijiji mbalimbali vya kata hiyo ikiwemo Kwamduma visima viwili, kibindi viwili, na Kwamsanja kimoja ambavyo vimesaidia kidogo japo shida bado haijaisha. 

,"...Uchimbaji wa mabwawa haya makubwa na usambazaji kwenda kwa wananchi unakuja wakati muafaka, hivyo matarajio ni kwenda kutatua shida ya Maji kwa ukubwa huo uliokusudiwa. 

Kwa hakika tuna kiongozi ambaye sio anasema mdomoni kuwajali wananchi wanyonge isipokuwa anatenda kwa vitendo pia Rais wetu Dkt. Magufuli."

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Bi. Zainab Kawawa akizungumza mbele ya wananchi wa kijiji cha Kwamduma alieleza kuwa, Serikali imejidhatiti kuhakikisha maji yanawafikia wananchi wa Kibindu hivyo alimuhakikishia Mbunge na wananchi kuwa mradi utakamilika mapema ili wananchi wapate maji safi na salama.

Akieleza juu ya Utekelezwaji wa Miradi huo, alisema Serikali imetoa Bilioni 1.6 kwa ajili ya Miradi yote ikiwemo Milioni 700 kwa ajili ya Kwamsanja na Milioni 900 kwa ajili ya Mjembe.

Ambapo miradi hiyo inatarajiwa kwa pamoja kutoa lita zisizo pungua Milioni Tatu na Nusu wingi ambao unakwenda kutatua kero ya Maji katika kata ya Kibindu.

Miradi hiyo itakapokamilika inataraji kuhudumia watu wanaoishi katika eneo la Kibindu na vitongoji vya Kata hii na za jirani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments