DED TINDWA AAHIDI KUTOA TAULO ZA KIKE SHULE YA SEKONDARI NYAMWAGA


Aliyevaa kofia nyeusi ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa akizungumza wakati wa Ziara ya Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini ya kutembelea miradi ya maendeleo.
Aliyevaa shati la Kitenge ni mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akimsikiliza Mwalimu mkuu wa shule ya Sekondari Nyamwaga Mwita Nyambacha akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni la wasichana litakalogharimu sh.milioni 80 fedha za Serikali

***

Na Dinna Maningo,Tarime

Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime mkoani Mara Apoo Tindwa  ameahidi kutoa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike katika shule ya Sekondari Nyamwaga kata ya Nyamwaga.

Tindwa ametoa ahadi hiyo leo baada ya Wanafunzi wa kike kumuomba mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara kuwapatia msaada wa taulo za kike wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi ya ujenzi wa bweni la wasichana katika shule hiyo.

"Changamoto zingine ziko ndani ya uwezo wa mbunge ila hili la taulo za kike liko ndani ya uwezo wangu nawahaidi januari,2021shule zikifunguliwa nitawanunulia hizo taulo ondoeni shaka", alisema Tindwa.

Elizabeth Boniface ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo alisema kuwa endapo watapata taulo za kike zitawasaidia kwa kuwa baadhi ya wanafunzi wanatoka katika familia zisizo na uwezo ambazo haziwezi kutoa fedha za kununua taulo za kike.

Mkuu wa shule hiyo Mwita Nyambacha alisema shule ina wasichana 196 nakwamba Serikali imetoa milioni 80 kujenga Bweni la wasichana ambalo ujenzi umefikia hatua ya msingi.

"Bweni hilo litachukua wanafunzi 80,ujenzi umechelewa kutokana na ubovu wa barabara baada ya mvua kunyesha na kusababisha gari kushindwa kufika kutuletea vifaa kama saruji,mchanga barabara haipitiki,bweni hili likikamilika litasaidia wanafunzi wanaotoka mbali", alisema Nyambacha.

Hata hivyo Waitara aliwataka wananchi na kamati inayosimamia ujenzi kuhakikisha hakuna ubadhilifu wa fedha na majengo yajengwe kwa kiwango kinachohitajika nakwamba wale watakaoboronga kazi wasipewe kazi nyingine.

Mbunge huyo alikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa mawili katika shule ya Sekondari Nyamwigura kata ya Binagi ambapo ujenzi wake utagharimu shilingi. Milioni 46 na vyoo matundu 6, alikagua ujenzi wa kituo cha Afya Magoma na miradi mingine ukiwemo mradi wa ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Magoma utakaogharimu sh.Milioni 40.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments