WAITARA AWATAKA WANAFUNZI KUSOMA KWA BIDII,AMSHUKURU RAIS MAGUFULI KUMTEUA KUWA NAIBU WAZIRI


Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kebogwe kata ya Binagi
 
Na Dinna Maningo,Tarime

 Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri mteule Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira  amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii ili kufaulu vizuri katika mitihani yao. 

Waitara ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo akiwa ameambatana na baadhi ya watendaji wa halmashauri,Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Simion Samwel,Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Victoria Mapesa, Kamati ya siasa ya chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Tarime ikiongozwa na Katibu wa CCM Hamis Mkaruka. 

Waitara amekagua ujenzi wa maabara 3,Jengo la utawala na nyumba moja ya utumishi katika shule ya Sekondari Kebogwe kata ya Binagi ambazo  zinajengwa kwa sh.milioni 150 fedha za Serikali chini ya mpango wa Lipa kulingana na matokeo(EP4R). 

"Mwakani tutaweka mashindano shule zote kwenye jimbo langu zitakuwa zinafanya mitihani kwa kushindana kwa kufanya mitihani,shule zitakazokuwa zikishinda tutazipa zawadi hatutaki kuona mnavaa sare mnapendeza alafu kwenye mitihani mnapata sifuri", amesema Waitara.

Mkuu wa shule ya Sekondari Kebogwe Leonard Isaya amesema kuwa ujenzi unaendelea na  haujakamilika kwa wakati kutokana na  kunyesha kwa mvua iliyosababisha miundimbinu ya barabara kuharibika na kusababisha vifaa vya ujenzi kutofika kwa wakati. 

Waitara ametembelea na kukagua ujenzi wa bweni la wasichana shule ya Sekondari Nyamwaga ambao utagharimu fedha milioni 80. 

Mbunge huyo amezungumza na wanafunzi ambao nao walitoa kero zao ikiwemo maabara moja kutokuwa na vifaa vya kutosheleza,ukosefu wa mwalimu wa hesabu,vitabu vya sanaa  vikiwemo vitabu vya historia na ameahidi kuzifanyia kazi changamoto hizo.

Wakati huo huo, Mbunge huyo amemshukuru Rais John Magufuli kwa kumteua kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira.

Waitara ametoa shukrani hiyo leo wakati akikagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Kebogwe kata ya Binagi wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo.

Waitara ameahidi kuchapa kazi huku akiahidi kutoa ushirikiano kwa wananchi katika kuhakikisha jimbo la Tarime vijijini linapata maendeleo.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa amempongeza Rais Magufuli kwa kumteua Waitara kuwa Naibu Waziri ambaye ni mbunge kutoka jimbo la Tarime vijijini lililoko katika halmashauri hiyo.
Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Kebogwe kata ya Binagi
Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara  ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira akizungumza  na wananchi waliokuwa kituo cha afya Magoma
Aliyevaa kofia nyeusi ni Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tarime Apoo Tindwa akizungumza jambo wakati wa Ziara ya Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini ya kutembelea miradi ya maendeleo.

Mbunge wa jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara  ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais,Muungano na Mazingira akisikiliza jambo kutoka kwa Diwani wa kata ya Binagi Marwa Marigiri wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi katika kata hiyo.
Mkuu wa shule ya Sekondari Nyamwigura Antony Ryoba akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments