WAANDISHI WA HABARI WAKUMBUSHWA KUANDIKA HABARI ZA KULINDA AMANI BAADA YA UCHAGUZI


Waandishi wa habari wametakiwa kuandika habari za kujenga Amani nchini na kuacha kupendelea kuandika habari za uchochezi na zenye kuleta taaruki.

Wito huo umetolewa leo na Mwezeshaji wa mafunzo ya kujenga Amani hasa baada ya Uchaguzi Denis Mpagaze yaliyoandaliwa na mtandao wa redio za kijamii nchini (TADIO)

Mpagaze amesema kuwa waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kujenga Amani nchini na kwamba taaluma yao inaweza kujenga au kuharibu kwani jamii inaviamini sana vyombo vya habari.

Katika hatua nyingine Mpagaze amewataka waandishi wa habari kuacha kuandika habari kwa kutumia habari za mitandaoni zenye mihemko na kwamba wafuate kanuni za uandishi kabla ya kusambaza habari zisizo na uhakika.

Mpagaze ameongeza kuwa yapo mambo mengi ya kuisaidia jamii na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya Amani na maendeleo na kuwataka waandishi kuacha kuandika habari zenye kuleta taharuki na kuleta hisia hasi kwa jamii.

Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo kutoka mtandao wa Redio za kijamii nchini Cosmas Lupoja amewataka washiriki kuzingatia mafunzo hayo na kuwataka waende kuyatumia katika vituo vyao ili kujenga Amani na kuwa kichecheo cha kuleta maendeleo nchini.

Nao baadhi ya waandishi wanaoshiriki semina hiyo Elias Maganga kutoka Pambazuko Fm ya wilaya ya Kilombero na Mwanaidi Kopakopa kutoka Redio jamii Mtwara wameshukuru mtandao wa redio za kijamii nchini TADIO kutoa mafunzo hayo kwani yamekuja wakati mzuri na yatawasaidia katika kaundaa habari na vipindi vyao.

Mafunzo hayo siku tano yameshirikisha washiriki sabini kutoka Redio thelathini na nne za bara na visiwani pamoja na chama cha waandishi wa habari Pemba.

CHANZO- KAHAMA FM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments