RC SHIGELLA AITAKA TMDA KUTOA ELIMU ZAIDI KWA WANANCHI

MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella akizungumza wakati akifungua mafunzo ya ukaguzi wa dawa yaliyofanyika katika ukumbi wa  wizara ya afya hospitali ya Bombo kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga (RMO) Dkt Jonathan Bademu

Mratibu wa Ofisi za Kanda na Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Henry Irunde akizungumza jambo wakati wa mafunzo hayo

MKUU wa Mkoa wa Tanga Martine Shigella ameitaka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kuhakikisha wanatoa elimu zaidi kwa wananchi ili waweze kufahamu ubora wa dawa sambamba na kuzingatia muda wa mwisho wa matumizi hususani maeneo yaliyopo mipakani.

Shigella aliyasema hayo wakati wa akifungua mafunzo ya ukaguzi wa dawa yaliyofanyika katika ukumbi wa  wizara ya afya hospitali ya Bombo ambapo amesema kuwa hata wananchi wanawajibu wa kutambua  dawa hizo na wakijiwekea utamaduni wa kusoma ili kutambua muda wa matumizi ya dawa hizo. 

Alisema kwamba iwapo wananchi wakipatiwa elimu hiyo itawasaidia kwani mtumiaji mmoja mmoja akinunua dawa na akajenga utamaduni wa kusoma na kujua muda wa matumizi ya dawa yenyewe itasaidia kutambua ambazo zimekwisha muda wake ambazo hazina ubora.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwamba kila kifaa tiba na kila aina ya dawa kabla haijaingia kwenye matumizi lazima mamlaka hiyo ijiridhishe ubora wake kama unakidhi mahitaji ya binadamu na iweze kusajiliwa na kuingia kwenye soko rasmi. 

“Kama kuna dawa yoyote ambayo inatumika au kifaa tiba ambacho kinatumika na hakijasajiliwa na TMDA hakuna maelezo mengine zaidi ya kusema hawa ni wahujumu uchumi kama wahujumu uchumi wengine." Alisema Shigella.

Awali akizungumza, Mratibu wa Ofisi za Kanda na Serikali za Mitaa, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Henry Irunde amesema kuwa katika Mkoa wa Tanga pamoja na udhibiti kwenye vituo vya forodha na soko umeimarishwa. 

Irunde amesema kuwa bado kuna changamoto ya uwepo wa dawa ambazo hazijasajiliwa na baadhi ya maduka ya dawa kutokuwa na vibali ikiwemo kukosa wataalamu wenye sifa stahili hivyo maduka hayo yanapaswa kukaguliwa mara kwa mara ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria.

Pia amesema kuwa mafunzo hayo yamezingatia masuala muhimu kwa wakaguzi ikiwa pamoja na kuwakumbusha wakaguzi juu ya maadili na taratibu za kazi katika kutimiza majukumu yao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post