WANAFUNZI 47,305 WAPANGIWA MIKOPO KATIKA AWAMU YA KWANZA

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya Awamu ya Kwanza yenye wanafunzi 47,305 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 150.03 bilioni kwa mwaka wa masomo 2020/2021 unaotarajiwa kuanzia wiki ijayo.

Akitangaza orodha hiyo leo (Jumatano, Novemba 11, 2020) jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema kuwa kati ya wanafunzi hao (47,305), wanaume ni 26,964 sawa na asilimia 57.37 na wanawake ni 20,341sawa na asilimia 42.63.

Badru ameongeza kuwa HESLB imeanza kupeleka fedha za wanafunzi waliopangiwa mikopo katika vyuo mbalimbali na kuwataka wanafunzi kupata taarifa za kina katika akaunti walizotumia kuomba mkopo maarufu kama SIPA (Student’s Individual Permanent Account) na kujiandaa kwenda vyuoni kwa ajili ya kujisajili.

“Serikali imeshatupatia fedha na tumeanza kuzipeleka vyuoni … lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanazikuta fedha vyuoni ambako watajisajili na kupokea ili watimize ndoto zao,” amesema Badru katika mkutano uliofanyika katika ofisi za HESLB jijini Dar es salaam.

Kuhusu kutangazwa kwa orodha ya Awamu ya Pili, Badru amesema imepangwa kutolewa Jumamosi, Novemba 14, 2020 baada ya kukamilisha uchambuzi wa maombi unaoendelea na kuwataka waombaji mikopo kutembelea akaunti zao ya SIPA kupata taarifa kuhusu maombi yao.

“Wanafunzi hawa wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mkopo kwa kuwa wana sifa zikiwemo kuwa wahitaji, wameomba kwa usahihi na wana udahili wa chuo kimoja … tunakamilisha uchambuzi wa maombi mengine na tutaoa orodha ya pili katika siku mbili zijazo, yaani Jumamosi, Novemba 14,” amesema Badru.

Aidha, katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa wanafunzi wenye mikopo wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini wapatao 44,629 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 155.06 bilioni.

“Wanafunzi hawa 44,629 wamepangiwa mikopo baada ya HESLB kupokea matokeo ya mitihani yanayothibitisha kuwa mwanafunzi amefaulu kuendelea na masomo katika mwaka unaoanza,” amesema Bw. Badru na kufafanua HESLB inaendelea kupokea matokeo ya wanafunzi waliokua na mikopo mwaka wa masomo uliopita na watapangiwa mikopo.

Katika mkutano huo, Bw. Badru ameeleza kuwa Serikali imetenga TZS 464 Bilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi 145,000ambapo kati yao, wanafunzi 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na TZS 91,000 ni wanafunzi wenye mikopo na wanaoendelea na masomo baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka. 

MWISHO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post