TAKUKURU SHINYANGA YAREJESHA MAMILIONI YA FEDHA ZA WALIMU WASTAAFU WALIOATHIRIKA NA MIKOPO UMIZA


Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Oktoba 20,2020 . Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Muonekano wa fedha za Walimu Wastaafu walioathirika na Mikopo Umiza na mwananchi aliyedhulumiwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mwanza akiwa katika harakati za kutafuta huduma ya kupimiwa shamba lake.
Kulia ni Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga , Francis Luena akimkabidhi Mwalimu Mstaafu Elias Mihambo Katinda kiasi cha shilingi 8,100,000/= aliyeathirika na Mikopo Umiza ambapo  fedha zingine zilizobaki shilingi 18,200,000/= zinaendelea kurejeshwa.
Kulia ni Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga , Francis Luena akimkabidhi Mwalimu Mstaafu Hamis Maziku Chaba kiasi cha shilingi 8,500,000/= aliyeathirika na Mikopo Umiza ambapo  fedha zingine zilizobaki kiasi cha shilingi 11,000,000/= zinaendelea kurejeshwa.
Kulia ni Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga , Francis Luena akimkabidhi mwananchi  Gasto Njau aliyedhulumiwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mwanza akiwa katika harakati za kutafuta huduma ya kupimiwa shamba lake kiasi cha shilingi shilingi 10,400,000/=.

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Shinyanga imefanikiwa kurejesha Shilingi Milioni 27 za Walimu Wastaafu walioathirika na Mikopo Umiza na mwananchi aliyedhulumiwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Mwanza akiwa katika harakati za kutafuta huduma ya kupimiwa shamba lake.

Akitoa Taarifa kwa Vyombo vya Habari leo Jumanne Oktoba 20,2020 na Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Hussein Mussa amesema katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2020,wamerejesha fedha hizo jumla ya shilingi 27,000,000/=.

“Katika fedha hizo kiasi cha shilingi 16,600,000/= ni za walimu wastaafu wawili ambao ni Elias Mihambo na Hamis Chaba walioathirika na mikopo umiza kutoka Kampuni mbalimbali zikiwemo za Malicha Microcredit C.Ltd, Kyanyari CO. Ltd na Mwalimu wa shule ya Sekondari Ibisageni na Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kahumulo wilayani Sengerema”,amesema Mussa. 

“Fedha zingine kiasi cha shilingi 10,400,000/=  ni za mwananchi aitwaye Gasto Njau aliyedhulumiwa kwa kuambiwa atoe fedha na Kamishna Msaidizi wa Ardhi kwa mkoa wa Mwanz kwa ajili ya kupimiwa eneo (shamba) lakini hakupatiwa huduma hiyo ya kupimiwa eneo lake”,ameeleza.

Amefafanua fedha za Mwalimu Mstaafu Elias Mihambo Katinda zilichochukuliwa isivyo halali ni shilingi Milioni 45 ambapo tayari kiasi cha shilingi Milioni 18.5 zilikabidhiwa kwa mstaafu husika awamu ya kwanza Julai 24,2020 na leo amekabidhiwa kiasi cha shilingi 8,100,000/= na fedha zingine zilizobaki shilingi 18,200,000/= zinaendelea kurejeshwa.

“Fedha za mwalimu mstaafu Hamis Maziku Chaba zilizochukuliwa isivyostahili ni shilingi 27,500,000/= ambapo tayari kiasi cha shilingi 8,000,000/= zilikabidhiwa kwa mstaafu huyo awamu ya kwanza Julai 24,2020 na leo tunamkabidhi kiasi cha shilingi 8,500,000/=, fedha zingine zilizobaki kiasi cha shilingi 11,000,000/= zinaendelea kurejeshwa”,ameongeza Mussa.

Kuhusu mwananchi  Gasto Njau aliyetoa kiasi cha shilingi 10,400,000/= kwa kamishna msaidizi wa ardhi mkoa wa Mwanza kwa ajili ya kupimiwa eneo (shamba) lake lililopo katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga katika kijiji cha Pandagichiza lenye ukubwa wa ekari 23 pamoja na kupatiwa hati miliki mwezi Oktoba 2019 lakini mpaka mwaka huu hajapimiwa wala kupewa hatimiliki ambapo fedha hizo zimeshalipwa na kamishna huyo.

“Kutokana na muundo wa Idara ya Ardhi hivi sasa mkoa wa Shinyanga una Kamishna wa Ardhi hivyo TAKUKURU ilimtaka kamishna huyo kurejesha fedha hizo ili mwananchi huyo aendelee na taratibu  za kupimiwa eneo lake kwa kutumia ofisi ya kamishna wa ardhi wa Shinyanga kama atahitaji kuendelea na zoezi hilo na leo tumemkabidhi mwananchi huyo fedha zake zote shilingi 10,400,000/=”,ameongeza Mussa.

Kwa upande wao, Walimu hao wastaafu na mwananchi huyo wameishukuru TAKUKURU kazi nzuri inayofanya katika kusimamia haki kwa kufanikisha kurejeshewa fedha zao.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments