SIKONGE YATAKIWA KUPIMA MASHAMBA YA WANAVIJIJI AMBAO HAWAJAPIMIWA


NA TIGANYA VINCENT
HALMASHAURI ya Wilaya ya Sikonge imetakiwa kuhakiki na kupima mashamba ya wanavijiji ambayo hayajapimwa ili waweze kupatiwa hati ya hakimiliki ya kimila kwa ajili ya kuyaongezea thamani.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Sikonge Peres Magiri wakati akikabidhi hati ya hakimiliki ya kimila za awamu ya pili 224 kwa Vijiji vitatu na hivyo kufikisha Hati 856 ambazo zimekwishatolewa chini Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania(MKURABITA).

Alisema hatua hiyo itasaidia kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao utasaidia kuondoa migogoro miongoni mwa wanavijiji wao kwa wao.

Magiri alisema kuwa Wilaya ya Sikonge ina Vijiji 71 lakini ambavyo wakazi wamepimiwa maeneo yao ni 12 na kubaki 59, jambo ambalo linahitaji kufanyia kazi ili kukamilisha vyote.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanatatua tatizo la mwingiliano wa maeneo 102 katika Vijiji vya Ukondamoyo, Mole na Usanganya ambalo ulisababisha MKURABITA washindwe kuandaa hati za Hakimiliki za Kimila kwa wananchi.

Alisema sanjari na hilo ni vema wanakijiji 797 ambao hawakujitokeza wakati MKURABITA wakihakiki maeneo katika vijiji vyao wajitokeza ili nao waweze kupimiwa maeneo yao kwa ajili ya kupatiwa hati.

Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Dkt. Seraphia Mgembe aliwataka wanavijiji kuhakikisha wanatumia Hati ya Hakimiliki za Kimila wanazopatiwa kuendesha kilimo na biashara zao kwa tija ili kuchangia katika maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Alisema hati hizo walizopewa ni mtaji ambao wanatakiwa kuutumia kujiongeza kipato kwa kuandaa mipango mizuri ambao itawawezesha kunufaika na fursa ya mikopo katika Taasisi za Fedha.

Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) hadi hivi sasa umesharasimisha rasilimali na biashara za wanyonge katika Wilaya 52 kwa upande wa Tanzania bara.
MWISHO


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments