Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dkt. Hussein Ali Mwinyi Aahidi Kutokomeza Ubaguzi Zanzibar


Mgombea  Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dkt. Hussein Ali Mwinyi,ameahidi kupambana na vitendo vyote vya ubaguzi ndani ya jamii pindi akipata ridhaa ya kuongoza Zanzibar.

Amesema ili kutokomeza vitendo vya ubaguzi visiwani humo, lazima akiri na kukubali kuwa vitendo hivyo vipo, kisha achukua hatua ya pili ya kutokomeza vitendo hivyo.

Dkt. Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na viongozi na waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini ya Kikristo Zanzibar katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul Wakil Kikwajuni, leo.

Amesema nchini kuna ubaguzi wa dini,ubaguzi wa kijinsia,ubaguzi wa kikanda wa Ubara, Uunguja na Upemba na yote hayo yanatakiwa kutokomezwa.

Amesema changamoto hizo zikiondolewa Zanzibar itaimarika kwa kasi kiuchumi, kijamii na kisiasa. Alisema viongozi na waumini wa dini ni wadau wakubwa wa maendeleo, hivyo wanatakiwa kutoa mchango wao katika maendeleo ya nchi.

Dkt. Mwinyi amesema lengo lake kugombea urais ni kutaka kuwaletea wananchi wa makundi yote maendeleo endelevu.

Alisema dhamira yake ni njema ya kuwatumikia wananchi wote, kwani kiongozi yeyote anayetafuta uongozi mkubwa wa nchi hawajibiki kwa wale wanaompigia kura tu, bali anawajibika hata kwa Mungu.

Amesema katika uongozi wake atahakikisha anatenda haki kwa makundi yote. Pia aliahidi kusimamia haki ya kikatiba ya kuhakikisha kila mtu anapata uhuru wa kuabudu dini anayoiamini ili nchi ibaki kuwa salama.

Alitumia nafasi hiyo kujiombea kura na kuwaombea wagombea wote wa CCM ili chama kishinde na kuendelea kuongoza dola.Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments