MAJALIWA : HATUWEZI KUWAACHA WASANII


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali ijayo ya CCM itaendelea kuwaunga mkono na kuwaendeleza wajasiriamali wakiwemo wasanii.

"Serikali ya CCM inawathamini sana wasanii kwa sababu sanaa ni sawa na ujasiriamali. Kwa maana hiyo, sanaa ni ajira," alisema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Oktoba 2, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa wilaya ya Kahama katika mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Magufuli mjini Kahama, mkoani Shinyanga.

Akielezea kuhusu ujenzi wa barabara za kuunganisha mikoa, Mheshimiwa Majaliwa alisema kwenye ilani ya uchaguzi, barabara kubwa inayotajwa kuunganisha mji wa Kahama na mikoa ya jirani ni ya kutoka Katavi hadi Tabora kupitia Ugalla.

"Katika uk. 73, Ilani yetu inataja barabara zinatotakiwa kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami ambazo ni Mpanda - Ugala - Kaliua - Ulyankulu - Kahama (km 428); Geita – Bukoli – Kahama (km 107) na Kahama – Nyamilangano – Uyogo (km 54).”

Mheshimiwa Majaliwa ambaye amemaliza ziara yake ya kumuombea kura mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alimnadi pia mgombea ubunge wa jimbo la Kahama mjini, Bw. Jumanne Kishimba na wagombea udiwani wa wilaya hiyo.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Madini, Bw. Dotto Biteko alisema wilaya ya Kahama imepanda chati ya makusanyo yatokanayo na madini kutokana na usimamizi wa Serikali ya awamu ya tano.

"Kwenye makusanyo ya madini, Kahama ilikuwa ikishika nafasi ya nne. Sasa hivi imepanda na kuchukua nafasi ya pili. Mnashindana na Geita. Chunya ndiyo ilikuwa ikishika nafasi ya pili, lakini sasa hivi mmeiacha mbali. Chagueni viongozi wa CCM ili iendelee kuwaletea neema," alisema.



 

(mwisho)



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527