SHIRIKA LA YOUNG WOMEN LEADERSHIP LATOA MAFUNZO YA LISHE KWA WATOA HUDUMA YA AFYA NGAZI YA JAMII MWAWAZA | MALUNDE 1 BLOG

Thursday, October 1, 2020

SHIRIKA LA YOUNG WOMEN LEADERSHIP LATOA MAFUNZO YA LISHE KWA WATOA HUDUMA YA AFYA NGAZI YA JAMII MWAWAZA

  Malunde       Thursday, October 1, 2020

Afisa Miradi wa Shirika la Young Women Leadership (YWL), Veronica Massawe akizungumza wakati wa mafunzo ya lishe kwa watoa huduma ya afya ngazi ya jamii kutoka Kata ya Mwawaza katika Manispaa ya Shinyanga.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Shirika la Young Women Leadership ‘YWL’ linalojihusisha na utetezi wa haki za wanawake, vijana na watoto limetoa mafunzo ya lishe kwa watoa huduma ya afya ngazi ya jamii ili waweze kuelimisha wazazi au walezi wenye watoto kuanzia mwaka 0 hadi 6 kwa lengo la kuimarisha kinga ya mwili na afya kwa watoto chini ya umri wa miaka 6.

Akizungumza leo Alhamis Oktoba 1,2020 wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Shinyanga Fairies Hotel, Afisa Lishe wa Manispaa ya Shinyanga, Joanitha Jovin aliwataka watoa huduma ya afya ngazi ya jamii kufikisha elimu hiyo kwa walengwa ili kuwasisitiza wazingatie lishe bora kwa watoto wao.

“Kupitia mafunzo haya nendeni mkawaelimishe wazazi na walezi wenye watoto kuanzia mwaka 0 hadi 6 mliowabaini kupitia  kaya hadi kaya kwenye maeneo yenu kuhusu njia rahisi na rafiki za kuimarisha lishe bora kwa akina mama wajawazito,wanaonyonyesha na wenye watoto chini ya umri wa miaka 6”,alisema Joanitha.

Naye Afisa Miradi wa Shirika la Young Women Leadership (YWL), Veronica Massawe amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa "Uwajibikaji Jamii kwa watoto na familia" (Community Action For Children and Families) unaotekelezwa na YWL katika vijiji vitatu vya Kata ya Mwawaza ambavyo ni Mwawaza, Negezi na Bugimbagu kwa muda wa mwaka mmoja (Agosti 2020 – Julai 2021) kwa ufadhili Shirika la Firelight Foundation la nchini Marekani.

Alisema lengo la mradi huo ni kuziwesha familia 600 katika kaya ya Mwawaza ili kuimarisha kinga ya mwili,afya ya watoto na familia pamoja na  uchumi wa familia kwa kuwawezesha kuanzisha na kuendeleza kilimo cha vyakula lishe ikiwemo matunda na mbogamboga ambapo walengwa ni wazazi au walezi wenye watoto kuanzia umri wa mwaka 0 hadi miaka 6.

“Miongoni mwa majukumu ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii ni kuwafuata walengwa wa mradi kaya hadi kaya na kuwaelisha kuhusu lishe kwa wajawazito na wanawake wanaonyesha,unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee ndani ya miezi 6 ya mwanzo ili kuimarisha kinga ya mwili na afya ya mtoto na vyakula vya nyongeza kwa mtoto kuanzia miezi 6 ya mwanzo”,alifafanua Veronica.

Alisema elimu nyingine ni kuhusu usafi na usalama wa maji na mazingira,malezi na makuzi bora ya mtoto na masuala ya kijinsia katika malezi ya mtoto sambamba na kuwafundisha na kuwaanzishia bustani za mboga mboga,matunda na vyakula lishe ili kuimarisha lishe kwa watoto wenye umri chini ya miaka 6 na kukuza kipato cha familia.
Afisa Lishe wa Manispaa ya Shinyanga, Joanitha Jovin akitoa elimu ya lishe wakati wa mafunzo ya lishe kwa watoa huduma ya afya ngazi ya Jamii kutoka Kata ya Mwawaza katika Manispaa ya Shinyanga leo Oktoba 1,2020.
Afisa Lishe wa Manispaa ya Shinyanga, Joanitha Jovin akitoa elimu ya lishe wakati wa mafunzo ya lishe kwa watoa huduma za afya ngazi ya Jamii kutoka Kata ya Mwawaza katika Manispaa ya Shinyanga.
Afisa Miradi wa Shirika la Young Women Leadership (YWL), Veronica Massawe akizungumza wakati wa mafunzo ya lishe kwa watoa huduma za afya ngazi ya Jamii kutoka Kata ya Mwawaza katika Manispaa ya Shinyanga.

Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post