Majaliwa: Tupeni Kiongozi Atakayekuza Mahusiano Na Jirani


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Tanzania inahitaji kuwa na kiongozi ambaye atakuza mahusiano na nchi jirani.

“Tanzania inazungukwa na nchi tisa ambazo baadhi yake ziko kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki na nyingine hazimo. Tunahitaji kiongozi ambaye ataweza kuhakikisha nchi hii inakuwa na mahusiano mema na nchi jirani na nchi nyingine duniani kote lakini pia anaweza kuilinda heshima ya nchi yetu,” amesema.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Oktoba mosi, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Nyakahura na Nyakanazi, wilayani Biharamulo, mkoani Kagera akiwa njiani kuelekea wilaya za Bukombe na Mbogwe mkoani Geita.

Mheshimiwa Majaliwa ambaye ambaye amemaliza ziara yake mkoani Kagera ya kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli alitumia fursa hiyo kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Biharamulo Magharibi, Eng. Ezra Chiwelesa na wagombea udiwani wa CCM wa kata hizo, Apolinary Mgalula na Amos Madegwa.

Akielezea suala la vitambulisho vya uraia, Mheshimiwa Majaliwa amesema kote alikopita mkoani humo wananchi wanaulizia kuhusu uchelewaji wa kutolewa kwa vitambulisho hivyo. “Ucheleweshaji huu hauko hapa mkoani Kagera tu bali hata kwenye mikoa ya pembezoni ya Kigoma, Songwe, Katavi, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Pwani, Arusha na Mara”

“Hii ni kwa sababu tunataka tujiridhishe na uraia wa waombaji kwani hili suala ni kwa usalama wa nchi yetu. Wale walioko jirani umbali wa km. 10 wanaruhusiwa kuja kutembea au kufanya biashara na kurudi kwao. Hawaruhusiwi kupata vitambulisho, hivi ni kwa Watanzania tu.”

Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia wakazi hao kwamba kila Mtanzania mwenye sifa atapata kitambulisho cha Taifa kwa kuwa ndiyo mkakati wa Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Uhamiaji inatakiwa kuwa makini kusimamia mchakato huo kwa sababu wapo baadhi raia wa nchi jirani wanatamani kupata kitambulisho cha Taifa kutokana na amani iliyopo nchini. “Uhamiaji iwe makini haitapendeza kuona Mtanzania anakosa kitambulisho cha Taifa halafu mgeni kutoka nchi jirani anapata,” amesema.

Hata hivyo, amewataka wakazi hao wasikubali kutoa rushwa kwa sababu hiyo ni haki yao na kwamba endapo itatokea kuwa wameombwa rushwa watoe taarifa. “Mtu wa uhamiaji akidai rushwa ili akupatie kitambulisho toa taarifa mara moja ili tumshughulikie,” amesisitiza.


Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments