WAZIRI WA NISHATI DK. KALEMANI : HAKIKISHENI UMEME HAUKATIKI WAKATI WOTE WA UCHAGUZI MKUU


Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (wakwanza kushoto) akiongozana na MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme nchini TANESCO Mhandisi Tito Mwinuka (wakwanza kulia) na Meneja mraadi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme Cha Dege wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam, Mhandisi Neema Mushi (katikati mbele) wakati wa ziara ya Waziri huyo alipotembelea kituo hicho Oktoba 17, 2020.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani alisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea kituo cha kupoza na kusambaza umeme Dege wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam Oktoba 17, 2020. Alisema ujenzi wa kituo hicho chenye uwezo wa Megawati 48 umefikia asilimia asilimia 81 na ujenzi utakamilika Novemba mwaka huu 2020.
Miundombinu ya kupokea nyaya tayari ikiwa imekamilika.
Transfoma yenye ukubwa wa Megawati 48 tayari imefungwa.
Mhandisi mzalendo kutoka TANESCO kiwa kazini.
Dkt. Kalemani akiagana na mkandarasi
Dkt. Kalemani akijadiliana jambo na viongozi wa TANESCO na wa Wizara wakati akijiandaa kuondoka eneo la ujenzi.
***

WAZIRI wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewataka Mameneja wa Shirika la Umeme nchini TANESCO wa ngazi za Kanda, Mikoa na Wilaya kuhakikisha umeme haukatiki katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu hususan siku ya kupiga kura. 

Dkt.Kalemani ameyasema hayo leo Oktoba 17, 2020 baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza na kusambaza umeme Megawati 48 cha Dege wilayani Kigamboni jijini Dar es Salaam. 

“Maeneo yote kuanzia kwenye vijiji, kata wilaya na mikoa nchi nzima umeme usikatike wakati wa uchaguzi, usikatike maeneo yote na muda wote lakini hasa hasa wakati wa kupiga kura tarehe 28, Oktoba, tunataka wananchi wapige kura kwa uhuru na uhakika.” Alisisitiza Dkt. Kalemani ambaye alifuatana na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt. Tito Mwinuka na viongozi wengine wa wizara. 

Akizungumzia kuhusu kituo hicho cha kupoza na kusambaza umeme cha Dege, Dkt. Kalemani alisema ujenzi wake umefikia asilimia 81 na amewaagiza wakandarasi kuhakikisha ifikapo Novemba 2020 ujenzi uwe umekamilika kwa asilimia 100. 

Alisema ametembelea kituo hicho mara sita na lengo ni kuhakikisha wananachi wa Kigamboni wanapata umeme wa uhakika wakati wote. 

“Niwapongeze TANESCO na Mkandarasi kwa hatua mliyofikia ingawa Mkandarasi aliomba miezi miwili kukamilisha kazi hii mimi nimesema hapana, kwanza kazi yenyewe iliyobaki ni ndogo hivyo nimetoa mwezi mmoja kufikia Novemba ujenzi uwe umekamilika.” Alisisitiza Dkt. KJalemani. 

Waziri aliwasifu wahandisi wazalendo kutoka TANESCO kwani mafundi wa kujenga kituo hiki ni TANESCO wenyewe Mkandarasi kutoka Crotia anasimamia tu na kutoka hapa tutakuwa tumepata ujuzi wa kutosha kuanza kujenga vituo vyetu sisi wenyewe na tayari tumeanza kule Tabora pamoja na Katavi wanasimamia na kujenga TANESCO wenyewe. Alisifu Dkt. Kalemani 

Aliisifu Serikali ya awamu ya tano kwa kuwekeza fedha nyingi kwenye miundombinu ya umeme kwani katika kipindi cha miaka mitano jumla ya vituo vya kupoza na kusambaza umeme vikubwa na vidogo 141 vimejengwa nchi nzima. 

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Meneja Mradi, Mhandisi Neema Mushi alisema mradi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 26. 2 ikijumuisha na ulipaji fidia kwa wakazi waliohamishwa kupisha mradi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments