TARI YATOA ELIMU KUDHIBITI MAGONJWA YA ZAO LA KOROSHO

 

Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa Visumbufu vya Wadudu na Magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Mtwara, Dkt.Wilson Nene, akiwaeleza  Maafisa Ugani na Wakulima namna  ugonjwa wa Ubwiriunga unavyoathiri mikorosho wakati wa mafunzo kwa vitendo yaliyofanyika Shule ya Sekondari ya Mnyakongo wilayani Kongwa mkoani Dodoma jana..

Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu,  akitoa mafunzo ya jinsi ya kupogolea  mkorosho ili uweze kustawi vizuri.
Maafisa Ugani na Wakulima wa Wilaya ya Kongwa wakiwa shambani wakijifunza namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali yanayoathiri mikorosho.




Mtafiti Mwandamizi na Mdhibiti wa Visumbufu vya Wadudu na Magonjwa kwenye zao la korosho, kutoka Tari- Naliendele  Mtwara, Dkt.Wilson Nene, akiwaeleza  Maafisa Ugani na Wakulima namna ya kudhibiti magonjwa mbalimbali ya zao hilo.


Moja ya mkorosho wilaya ya Kongwa ulivyoathiriwa na wadudu waharibifu.

Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu, akionesha namna ya kutumia mashine ya kupulizia (Motorized Blower).


Mtafiti wa Kilimo kutoka  Tari Naliendele, Selemani Libaburu, akimfundisha Mwalimu wa Kilimo wa Shule ya Sekondary ya Mnyakongo, Rehema  Lighola namna ya kutumia mashine ya kupulizia kwenye shamba la korosho.
Mwalimu wa Kilimo wa Shule ya Sekondary ya Mnyakongo, Rehema  Lighola akijifunza namna ya kutumia mashine ya kupulizia viuatilifu kwenye shamba la korosho.
Mkulima wa Kata ya Songambele, Richard Sanyaji,  akijifunza namna ya kutumia mashine ya kupulizia viuatilifu kwenye shamba la korosho.
 


Na Godwin Myovela, Kongwa Dodoma

KITUO cha Utafiti wa Kilimo TARI Naliendele hatimaye kimetoa majawabu ya namna ya kudhibiti visumbufu vya wadudu waharibifu na magonjwa, ikiwemo ugonjwa wa Ubwiriunga, ugonjwa wa Blaiti na Debeki ambayo kwa kiasi kikubwa yamekuwa ni changamoto kwa ustawi wa zao la korosho ndani ya Wilaya ya Kongwa na kwingineko nchini

Athari nyingine zilizoonekana wazi ndani ya wilaya hiyo na kupatiwa ufumbuzi na Tari Naliendele ni pamoja na kukithiri kwa wadudu waharibifu wa zao hilo wakiwemo Mbu wa Mikorosho, Mbu wa Minazi na Vidung’ata ambao ni kikwazo kikubwa cha ukuaji mzuri wa zao la Korosho ambalo linatajwa kuwa ni zao lenye uchumi mkubwa na soko la uhakika

Akizungumza kwenye mafunzo ya Kilimo Bora cha Korosho yaliyotolewa jana wilayani hapa kwa wakulima na Maafisa Ugani, Mtafiti kutoka TARI Naliendele Programu ya Korosho, Kitengo cha Udhibiti wa Visumbufu vya Wadudu waharibifu na Magonjwa, Dk Wilson Nene, alisema ugonjwa wa ubwiriunga kama usipodhibitiwa hugeuka tishio kwa ustawi wa mkorosho na  hasara yake ni kuanzia asilimia 70 mpaka 100 (kwa maana ya kutoambulia mavuno yoyote)

“Hapa Kongwa kwenye mashamba tuliyokwenda kufanyia ‘field’ tumeona kuna changamoto ya magonjwa kwa mikorosho mingi kuwa na matatizo ya wadudu waharibifu hasa mbu wa mikorosho, mbu wa minazi na ugonjwa wa ubwiriunga,” alisema Nene

Alisema wadudu hao wakiwa wengi na kushambulia kwa kasi husababisha majani ya mkorosho husika kuathirika, na zaidi majani yake hubadilika na kuonekana yameungua au mfano wa kitu kilichoungua au kubabuliwa na moto au moshi

“Hali hiyo hutokana na wadudu hawa waharibifu mbu wa minazi na mbu wa mikorosho wanapokuwa wanafyonza kwenye majani ‘maeneo teketeke’…basi pale walipofyonza inatokea vidonda ambapo ndio sehemu kimelea hicho kinachosababisha ugonjwa unaoitwa ‘Debeki’ kinapoingilia. Ndio maana hapa Kongwa tumekuta baadhi ya mikorosho imeathiriwa na Debeki,” alisema

Dk Nene alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wakulima wa Kongwa, na wengine waliopo mikoa yote 17 inayolima zao hilo nchini kwanza kutambua wadudu waharibifu na magonjwa ya mkorosho kabla athari hazijajitokeza lakini pia kuzingatia mafunzo ya namna ya kudhibiti kitaalamu yanayoendelea kutolewa na TARI kwa sasa

Alieleza kwamba kuna njia kuu tatu za kudhibiti ambazo ni njia za asili kwa maana ya usafi shambani, kuanzia katika upandaji-kupanda kwa nafasi, lakini pia mikorosho yako isisongamane ili kuweza kupogolea. Kwa kufanya hivyo mkulima atatengeneza mazingira yasiyo-rafiki kwa vimelea na wadudu hao waharibifu

Aidha, njia nyingine ni matumizi ya aina 54 ya mbegu bora zinazozalishwa na kituo cha utafiti wa kilimo Tari Naliendele, na kwa kufanya hivyo shamba la mkulima litakuwa na tija na ubora sambamba kuongezeka kwa kiwango cha uzalishaji bila kusahau matumizi sahihi ya viuatilifu na aina zake zote sanjari na matumizi bora ya mashine za kupulizia

“Kupitia elimu hii ambayo imekuwa na mwamko mkubwa tunaamini wilaya ya Kongwa na wakulima wengine za zao hili nchini sasa tutakwenda kuleta mchango mkubwa kwa kuongeza uzalishaji mara 4 kutoka kiwango cha sasa cha tani laki 3.15 kufikia tani milioni 1 kama shabaha ya taifa kufikia 2023.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments