KATIBU TAWALA MKOA WA SIMIYU ATAKA MIRADI YA MAENDELEO KUKAMILIKA KWA WAKATI

Ukamilikaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wakati kutarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu Bi. Miriam Mmbaga wakati alipofanya ziara ya kutembelea baadhi ya miradi ya Afya Wilayani Busega tarehe 9 Septemba, 2020, ambapo Bi. Mmbaga aliambatana na Timu ya Usamizi wa Huduma za Afya Ngazi ya Mkoa (RHMT).

Katika ziara hiyo ambayo Mmbaga alitembelea Hospitali ya Wilaya ya Busega ambapo alijionea ujenzi unaoendelea wa Njia za kupita Wagonjwa (Walk Ways) Mita 122 ambao unagharimu zaidi ya TZS Milioni 66.9, na ujenzi wa jengo la Theatre (Upasuaji) na Uzazi wenye thamani ya zaidi ya TZS Milioni 194.3. Mmbaga pia alitembelea ujenzi wa jengo la Upasuaji kituo cha Afya Lukungu, ujenzi unaofadhiliwa na AMREF kwa gharama ya TZS Million 142, na kusisitiza kukamilika kwa jengo hilo kwa wakati ili kuanza kutoa huduma za upasuaji kituoni hapo.

Kwa upande mwingine Mmbaga ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kwa kuwa mstari wa mbele katika miradi ya ujenzi wa miundombinu katika Hospitali ya Wilaya ya Busega kwa kuchangia fedha zinazotokana na mapato ya ndani na kumtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega Bw. Anderson Njiginya Kabuko kuendelea na utaratibu huo kwa kuongeza kiasi cha uchangiaji wa fedha. Namshukuru Mkurugenzi kuwa kipaumbele kwenye miradi kwani ameweza kuchangia ujenzi unaondelea na ninamtaka kuongeza zaidi uchangiaji na nampongeza sana, aliongeza Bi. Mmbaga.

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega, Anderson Njiginya Kabuko amemhakikishia Katibu Tawala wa Mkoa kuwa Ofisi yake itaendelea kuchangia fedha ili miradi ikamilike na kuanza kutoa huduma kwa wakati.

Kwa upande mwingine Mmbaga amewataka wafadhili na wadau wa maendeleo kukamilisha miradi wanayofadhili kwa wakati kwani miradi mingi imekuwa ikienda taratibu. Tunajua na tunatambua mchango wa wadau wa sekta ya Afya katika mkoa wetu lakini tunaomba wawe na utaratibu mzuri wa ufadhili wa miradi mbalimbali ili ikamilike kwa wakati, aliongeza Bi. Mmbaga.

Pia Mmbaga amewataka watumishi kuwa na ushirikiano ili kufanikisha huduma bora kwa wananchi. Watumishi mnatakiwa kuwa na ushirikiano ili kufikia malengo ya utoaji huduma, tutumie karama tulizopewa katika ufanyaji kazi, aliongeza Mmbaga. Kwa upande mwingine Mmbaga amempongeza Kaimu Mhandisi wa Ujenzi Wilaya ya Busega, Mhandisi. Paul Tumbu kwa juhudi na bidii ya uchapakazi katika miradi mbalimbali ya ujenzi Wilayani Busega huku akimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Busega kufuatilia uthibitisho wa cheo chake ili awe Mkuu wa Idara ya Ujenzi.

Awali Makamu Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Khamis Kulemba amewataka watumishi wa idara ya Afya kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi, na ameipongeza Timu ya Usamizi wa Huduma za Afya wilaya ya Busega (CHMT) kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Katika ziara hiyo pia Mmbaga alitembelea kikundi kinachojihusisha na kilimo cha umwagiliaji kinachojulikana kama Umoja wa Wamwagiliaji Nyakurunduma (UWANYA) na kuwataka wataalam wa kilimo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Busega kushirikiana na kikundi hicho na vingine kwaajili ya kutoa elimu ya uendeshaji na uzalishaji. Pia Mmbaga amevitaka vikundi vya kilimo cha umwagiliaji kutumia vyema rasilimali ya ziwa Viktoria.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post