MAKADA CCM RORYA WATAKA WANANCHI WACHAGUE VIONGOZI BILA KUJALI UKABILA…WAMUOMBEA KURA JAFARI CHEGE


Aliyekuwa Mbunge wa Rorya Lameck Airo akizungumza na wananchi wa kata ya Mirare wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea udiwani
***
Na Dinna Maningo, Rorya
Makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Rorya mkoani Mara  wamewaomba wananchi kutomchagua Mbunge kwa kigezo cha kabila lake bali wachague kiongozi ambaye atawaletea maendeleo huku wakiomba kumpigia kura Jafari Chege anayegombea ubunge Jimbo la Rorya kupitia CCM.

Akizungumza katika uzinduzi wa  kampeni za mgombea Udiwani kata ya Mirare Onyango Nyawambo,uliofanyika Septemba 13,2020 katika kijiji cha Ryagoro aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Lameck Airo na waliotia nia ya kugombea ubunge lakini kura zao hazikutosha  waliwataka wananchi kufanya maamuzi sahihi katika uchaguzi mkuu mwaka 2020 kwa kuchagua viongozi bila kujali makabila yao.

Airo aliwaomba wananchi kukipigia kura Chama cha Mapinduzi kwa kumchagua Dkt. John Pombe Magufuli,na wamchague Chege bila kujali kabila analotoka pamoja na diwani Nyawambo aliyezindua kampeni zake kwa kuwa kinachohitajika Rorya ni maendeleo na maendeleo hayana kabila.

Obuya Osogo aliyetia nia ya kugombea ubunge aliwataka wana Mirare kupiga vita ukabila na kwamba wagombea wasitumie ukabila kama ngazi ya kupitia kusaka Ubunge na Udiwani.

"Hatutaki habari za ukabila sisi sote ni wana Rorya wanaosaka uongozi  kwa kigezo cha ukabila tumpinge na tumkatae tunachotaka ni chama bora cha kutuongoza ambacho ni CCM ili kiendeleze kutekeleza Sera zake, Serikali ya CCM imetuletea umeme, vijiji kumi pekee ndiyo havijapata umeme tuna zahanati nyingi naomba tuichague tena ili iendelee kutatua changamoto zilizobaki", alisema Osogo.

Leonard Otuoma  aliwasisitiza wananchi kumpigia kura Chege na kwamba wakimchagua ataendelea kukomesha tatizo la wizi wa mifugo kama lilivyokuwa likidhibitiwa na Airo.

"Nawashukuru wajumbe kwa kunipigia kura hata kama hazikutosha tulikuwa wagombea 49 akashinda Chege na tumempatia ajenda zetu azifanyie kazi kuhakikisha Rorya inasonga mbele,yale yote tuliyowaambia tutayafanya wakati wa kuomba kura za maoni yatafanywa na Jafari", alisema Otuoma.

Frederic Magadi  mtiania Ubunge yeye alisisitiza kuwa maendeleo yanafanywa na CCM huku akiwataka vijana na Wanawake kuichagua CCM kutokana na kwamba Rais John Magufuli amekuwa akiwatetea wajasiliamali na kuhakikisha mikopo inatolewa ili kuwawezesha kujiinua kiuchumi.

Waliotia nia ya Udiwani katika kata hiyo na kutoshinda,Bosco Ojwan'g na Kefa Oliech ambaye pia alifanikisha ndugu yake Oguna Oliech wa Chadema kuhamia CCM walimuombea kura aliyeteuliwa  kugombea Udiwani na kuahidi kumpa ushirikiano kwenye kampeni.
Wa kwanza kulia ni Lameck Airo, katikati mgombea udiwani viti maalumu Ferista Awili na wa kwanza kushoto ni mgombea udiwani kata ya Mirare Nyawambo Onyango
Wananchi wakiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM
Aliyeshika kipaza sauti ni aliyekuwa mtia nia wa Udiwani Frola Patrick
Mwenyekiti wa CCM kata ya Mirare Timon Amara akimkumbatia Oguna Oliech aliyekuwa Chadema na kutimkia CCM wakati wa uzinduzi wa kampeni za mgombea udiwani
Mtiania Ubunge Leonard Otuoma akizungumza
Aliyekuwa Mtia nia ubunge Obuya Osogo akizungumza
Wananchi wa kata ya Mirare wakiwe kwenye kampeni za mgombea udiwani kata ya Mirare Nyawambo Onyango
Mbosco Ojwan'g mtiania Udiwani kata ya Mirare ambaye kura hazikutosha akizungumza
Bosco Ojwan'g mtiania Udiwani kata ya Mirare ambaye kura hazikutosha akizungumza
Kefa Oliechi mtiania Udiwani kata ya Mirare ambaye kura hazikutosha akizungumza

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527