Walioshindwa Kuzifuata Hati Za Ardhi Bunda Wamkera Naibu Waziri Mabula

Na Munir Shemweta, WANMM BUNDA
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameshangazwa na wananchi wa wilaya ya Bunda waliomilikishwa ardhi kushindwa kujitokeza kuchukua hati pamoja na kutangaziwa siku ya kukabidhiwa hati zao.

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanzisha utaratibu kupitia ofizi zake za mikoa kuwapelekea Hati wananchi karibu na maeneo yao ili kuwapunguzia usumbufu wa kuzifuata hati kwenye ofisi za mikoa.

Awali waliomilikishwa ardhi walitakiwa kusafiri umbali mrefu kufuata hati za ardhi ofisi za ardhi za kanda zilizokuwa zikihudumia mikoa zaidi ya mitatu jambo lililowafanya wamiliki hao kutumia gharama kubwa kufuatilia hati ofisi ya kanda.

Katika kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi pamoja na kupunguza gharama kwa wananchi kuzifuata huduma hizo kwa umbali mrefu  Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Julai mwaka huu imezindua ofisi za ardhi za mikoa zinazotoa huduma zote zilizokuwa zikitolewa katika ofisi za kanda. Huduma hizo ni pamoja na upimaji, uthamini, usajili na utoaji hati za ardhi pamoja na shughuli za mipango miji.

Akiwa wilayani Bunda jana katika ziara yake ya kikazi kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na miradi inayoendeshwa na Shirika la Nyumba la Taifa, Naibu Waziri Ardhi Dkt Mabula alishangazwa na idadi ndogo ya wananchi waliomilikishwa ardhi kujitokeza kuchukua hati zao  wilayani Bunda ambapo kati ya wamiliki 143 ni wamiliki sita (6) tu kati ya hao waliojitokeza kuchukua hati.

Naibu Waziri Mabula alisema, inashangaza kuona idadi ndogo ya wamiliki wa ardhi kujitokeza kuchukua hati wakati Wizara ya Ardhi imeamua kuwapelekea hati karibu na maeneo jambo linaloweza kuwasababisha kutumia gharama kuzifuata hati ofisi ya Msajili katika ofisi ya Ardhi mkoa wa Mara.

Katika ziara yake mkoani Mara Dkt Mabula alitembelea pia wilaya za Butiama, Tarime, Rorya na Musoma ambapo alizungumza na watumishi wa sekta ya ardhi katika wilaya hizo, kuangalia ukusanyaji kodi ya ardhi sambamba na kugawa Hati za Ardhi kwa wananchi waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments