Mashindano ya Masumbwi Kitaifa kufanyika Manyara

Na John Walter-Babati, Manyara
Kamati ya mchezo wa Masumbwi mkoa wa Manyara imeeleza kuwa mkoa huo umepewa heshma ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya kumtafuta bingwa wa ngumi kitaifa ambayo yatashirikisha vilabu vyote vya ngumi nchini vikiwemo vya majeshi ya ulinzi na usalama.
 
Mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti amesema, Shirikisho la ngumi Tanzania limeamua kuleta mashindano hayo makubwa katika mkoa wa Manyara ambayo yatafanyika kuanzia septemba 6,2020 katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati.
 
Amesema Mashindano hayo yatatanguliwa na pambano la mchujo Agosti 15 mwaka huu ili kupata wachezaji bora watakaounda timu ya mkoa wa Manyara itakayoshiriki Mashindano kitaifa.
 
Mkirikiti amewahakikishia washiriki wote wa ngumi nchini kuwa mkoa wa Manyara umejipanga vyema kuwapokea na kufanikisha jambo hilo la kitaifa kumpata bingwa.
 
Amesema ni fursa kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Manyara kujitokeza kudhamini na kutangaza biashara zao kupitia mashandano hayo makubwa yanayotarajiwa kuhudhuriwa na mamia ya watu kutoka kote nchini.
 
Kwa upande mwingine amewakumbusha wadau wote wa mchezo wa masumbwi watakaohudhuria mashindano hayo kutembelea mbuga za wanyama zilizopo katika mkoa huo,  Tarangire na Manyara kujionea vivutio mbalimbali.
 
Afisa Michezo mkoa wa Manyara Charles Maguzu amesema kuwa wamepata heshima hiyo kutokana na ulingo wa kisasa ambao upo katika mkoa huo pekee na ule wa jeshi .
 
Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya ngumi mkoa wa Manyara Bwana Nicolous Mwaibale amesema mpaka sasa maandalizi yanaendelea vizuri na kwamba timu ipo vizuri na itaingia kambini Jumatatu Agosti 10 ikiwa na wana masumbwi takribani 20.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments