NAIBU WAZIRI MABULA ATAKA MIKAKATI KUKAMILISHA UJENZI MRADI HOSPITALI YA KWANGWA

Na Munir Shemweta, WANMM MUSOMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa, Wizara ya Afya pamoja na Mshauri Mwelekezi wa mradi Chuo Kikuu cha Ardhi kukutana na kupanga mikakati kuhakikisha ujenzi mradi wa Hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara (KWANGWA) unakamilika kwa wakati.

Hatua hiyo inafuatia kusuasua kukamilika  ujenzi wa mradi huo unaogharimu takriban Shilingi bilioni 15.082 kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya mara kwa mara yanayotolewa na Mshauri Mwelekezi kwenye maeneo ya ujenzi wa mradi.

Dkt Mabula ametoa kauli hiyo jana alipotembelea mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara maarufu kama Kwangwa unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Mara pamoja na miradi inayofanywa na NHC.

Alisema, ujenzi wa mradi wa hospitali ya Rufaa mkoa wa Mara ni mzuri na ni wa kimakakati lakini kwa jinsi unavyoendelea unaweza usikidhi kiu na matakwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano John Magufuli kuona mradi huo unakamilika kwa wakati.

‘’ Nashauri pande zote tatu zikae tena na kuwekeana mikakati ya uhakika kuona  kazi inakamilika vipi na wanakwendaje katika kuhakikisha mradi huu unakamilika’’ alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, Mshauri Mwelekezi ambaye ni Chuo Kikuu cha Ardhi mara nyingi amekuwa hayuko kwenye eneo la ujenzi na amekuwa akileta mabadiliko katika ujenzi jambo alilolieleza kuwa linaongeza gharama na kurudisha nyuma kasi ya ujenzi.

Alisema, kutokuwepo eneo la ujenzi muda wote kwa Mshauri Mwelekezi kunasababisha ujenzi huo kuchelewa na baadhi ya kazi kufumuliwa upya kwa maelekezo ya mshauri jambo linalosababisha mradi kutoisha kwa wakati na kutaka Mshauri huyo kuwepo eneo la ujenzi muda wote ili kumfanya mkandarasi (NHC) asichelewe kumaliza kazi zake .

Dkt Mabula aliongeza kuwa, ratiba ya NHC ni kukamilisha Sehemu C ya mradi huo katika Jengo la Huduma ya Mama na Mtoto Agosti 15, 2020 lakini baadhi ya sehemu imeelekezwa kubomolewa wakati mkandarasi yuko hatua ya umaliziaji jambo linalofanya mradi kutokamilika kwa wakati.

Ameitaka Wizara ya Afya kumbana mshauri Mwelekezi ili aweze kufanya kazi yake vizuri ili Shirika la Nyumba la Taifa lifanye kazi yake bila kukwama na wakati huo lisiongeze gharama za ujenzi kwa kuwa Shirika linategemea fedha za miradi katika kujiendesha.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527