RAIS MAGUFULI AKAGUA MAGARI YALIYOTAIFISHWA BAADA YA KUHUSIKA KATIKA MATUKIO YA UHUJUMU UCHUMI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli leo amekagua magari yaliyotaifishwa baada ya kuhusika katika matukio ya uhujumu uchumi na kisha kuhifadhiwa katika kituo cha mabasi cha zamani Jijini Dodoma.


Idadi ya magari hayo ni 130 yakiwemo makubwa na madogo yalikamatwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini, kisha wahusika kufikishwa Mahakamani na Mahakama kutoa uamuzi wa kuyataifa.

Akizungumza baada ya kuyakagua, Rais Magufuli ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Jeshi la Polisi na wote waliohusika kuwakamata waliokuwa wanajihusisha na vitendo hivyo (ikiwemo biashara haramu ya meno ya tembo) na ameagiza magari hayo yagawanywe katika taasisi mbalimbali za Serikali ili yatumike kuendesha shughuli za kuwahudumia wananchi na kuzalisha mali.

Mhe. Rais Magufuli pia amewapongeza wananchi waliojitokeza kutoa taarifa zilizosaidia kukamatwa kwa watu waliokuwa wanafanya uhalifu kwa kutumia magari hayo na amewaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kukomesha vitendo hivyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527