POLISI WAKANUSHA KUTEKWA KWA KATIBU WA CHADEMA RUANGWA



Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi limekanusha taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Katibu  wa CHADEMA wa wilaya ya Ruangwa, Bw. Claudio Teodori Chilemba ametekwa.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ofisi ya Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Ruangwa leo Agosti 24, 2020, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Stanley Kulyamo amesema hakuna taarifa zozote za utekaji nyara kwa mtu huyo.

“Agosti 8, 2020 tulikuwa na taarifa za kutoweka na kwenda kusikojulikana kwa Katibu huyo ingawa hapo awali alimuaga Mwenyekiti wake kuwa anakwenda nyumbani kwake ila hakufanya hivyo. Jeshi la Polisi lilianza kufanya uchunguzi kuhusu kutoonekana  kwa Katibu huyo, Jeshi la Polisi kupitia kwa vyanzo vyake likagundua kuwa mtu huyo yupo wilayani Masasi Mkoa wa Mtwara “.

Kamanda Kulyamo amesema kuwa  Jeshi la Polisi liliwasiliana  na Msimamizi wa CHADEMA wa Kanda ya Kusini, Steward Ernest Kakingi ambaye alithibitisha kuwepo kwa katibu huyo wilayani Masasi  na aliahidi kumpeleka Kituo cha Polisi  kwa mahojiano akiwa na Mwanasheria wa Chama hicho ingawa hadi sasa hajafanya hivyo.

Amesema kuwa kupitia kwa wasiri wake, jana Agosti 23, 2020 Jeshi la Polisi lilipata taarifa kwamba Claudio Chilemba amekwishachukua fomu za kuwania kuteuliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea udiwani kata ya Chienjele  wilayani Ruangwa kwa tiketi ya CHADEMA.

Wakati huo huo, Kamanda Kulyamo amesema vijana watatu wamekatwa eneo la Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Ruangwa wakiwa na nondo mbili zilizoviringishwa bendera mbili za  Chama cha  ACT WAZALENDO pamoja na kisu kimoja na majina yao yamehifadhiwa.

Aidha, Kamanda Kulyamo amesema kuwa kati ya vijana hao, wawili wametoka Manispaa ya Lindi na mmoja ametoka Kata ya Mbekenyera ambapo kwa sasa wote watatu wako chini ya ulinzi wa jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi.

Kamanda Kulyamo alitoa wito kwa wananchi na viongozi wa vyama vya siasa kuacha kupotosha umma kwa taarifa za kuambiwa ambazo hawajazithibitisha na pia  sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko au taarifa zozote na uhalifu ni katika Jeshi la Polisi  ili  zipokelewe na kufanyiwa uchunguzi wa kina na hivyo kuliwezesha  jeshi  kuchukuwa hatua stahiki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527