MAREKANI YAIPONGEZA TANZANIA KWA KUDUMISHA AMANI NA DEMOKRASIA


Rais wa Tanzania, Mh. Dkt John Magufuli amepokea hati za utambulisho za mabalozi wawili walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao nchini Tanzania.


Waliowasilisha hati hizo Ikulu Jijini Dar es Salaam jana  Jumapili tarehe 2 Agosti 2020 ni, Dk. Donald John Wright, Balozi wa Marekani na Nguyen Nam Tien, Balozi wa Vietnam.

Taarifa iliyotolewa na Gerson Msigwa, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu imeaema, katika mazungumzo baada ya kupokea hati hizo, Rais Magufuli amewakaribisha mabalozi hao hapa nchini na ameeleza Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano mzuri na wa kihistoria uliopo kati yake na nchi hizo.

Rais Magufuli amewaomba mabalozi hao kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji kutoka nchini mwao kuja kuwekeza Tanzania na kwamba Serikali itakuwa tayari wakati wowote kutoa ushirikiano kwao.

Akizungumza baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho, Balozi Wright ameeleza kufurahishwa kwake na kurejea Tanzania baada ya miaka 33 tangu alipokuja kwa mara ya kwanza kufanya kazi za kutoa matibabu na kwamba tangu wakati huo anawaheshimu na kuwapenda Watanzania kutokana na ukarimu wao, upendo wao na jinsi wanavyoishi na wageni kama wanafamilia wao.

Balozi Wright amesema, Marekani inaiona Tanzania ni nchi imara, tulivu na yenye demokrasia na kwamba uhusiano wake mzuri na Marekani umeiwezesha kufanya kazi pamoja na anatarajia kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano zaidi na Serikali ya Tanzania.

Pia, Balozi Wright amewasilisha salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli kutoka kwa Rais wa Marekani, Donald Trump na Serikali ya Marekani kufuatia kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Hayati Benjamin William Mkapa na kueleza kuwa Marekani inatambua mchango mkubwa wa Hayati Mkapa kwa Tanzania na Kimataifa.

Naye, Nguyen Nam Tien amesema Tanzania ni nchi nzuri, Rais wake anafanya kazi nzuri na kwamba anatazamia kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu zaidi ili kukuza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Prof. Palamagamba Kabudi ameelezea uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Marekani na kwamba Marekani imekuwa ikifadhili miradi mingi ikiwemo afya  ambapo imetoa Sh. 1.56 Trilioni mwaka 2018, miradi 3,179 ya uwekezaji kutoka Marekani ambayo imezalisha ajira 550,000 kwa Watanzania, na pia mauzo ya bidhaa za Tanzania nchini Marekani yamekuwa yakiongezeka ambapo mwaka 2019 bidhaa zenye thamani ya Sh.119 Bilioni ziliuzwa nchini Marekani.

“Kwa hiyo uhusiano wa Tanzania na Marekani ni mzuri na unazidi kuimarika na tunaamini kuwa kuja kwa Balozi Donald John Wright kutaimarisha zaidi uhusiano huo” amesema Prof. Kabudi.

Kwa upande wa Vietnam, Prof. Kabudi amesema Tanzania imekuwa na uhusiano wa kidugu na kihistoria na nchi hiyo ambapo inashirikiana nayo katika mambo mengi ikiwemo uwekezaji wa kampuni ya simu za mkononi ya Halotel.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527