BUTONDO ARUDISHA FOMU ZA KUGOMBEA UBUNGE KISHAPU KWA KISHINDO....CCM YAAHIDI KUFANYA KAMPENI ZA KISTAARABU UCHAGUZI MKUU...


Wanachama wa CCM wakimsindikiza Mgombea Ubunge Jimbo la Kishapu Boniphace Nyangindu Butondo kurudisha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kishapu. Picha na Suzy Luhende.


Na Suzy Luhende - Kishapu
Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kimeahidi kuendesha kampeni za kistaarabu katika kipindi chote cha kampeni huku kikiwataka wanachama wake kutofanya vitendo vyovyote vyenye viashiria vya kuleta vurugu kipindi cha kampeni za kuwanadi wagombea udiwani na ubunge wa CCM.

Ahadi hiyo imetolewa leo Jumanne Agosti 25,2020 na Kaimu Katibu wa CCM wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Jamal Khamis wakati mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Kishapu, Boniphace Nyangindu Butondo akirejesha fomu zake kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Emmanuel Matinyi.

Khamis alisema Chama Cha Mapinduzi kitanadi kwa wananchi Sera na Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025 katika hali ya amani na utulivu ambapo kimetoa wito kwa wanachama wake kujiepusha na kutoa kwa watu wengine kauli zisizokuwa za kistaarabu zinazoweza kuwa chanzo cha kutokea kwa vurugu.

Ahadi hiyo ya CCM  ilionekana dhahiri baada ya wafuasi wa chama hicho na wale wa CHADEMA kuwasili wakati mmoja kwa msimamizi wa uchaguzi wakati wagombea wao wakirejesha fomu zao za kuomba uteuzi wa kugombea ubunge katika jimbo la Kishapu ambapo hakuna vurugu zozote zilizotokea.

“Tutafanya kampeni za kistaarabu zisizo kuwa na bughudha ambazo hazitashambulia mtu kampeni zenye malengo na kushawishi wapiga kura wetu waweze kutuchagua, tunaamini maendeleo msingi wake ni amani, pasipokuwa na amani hakuna maendeleo, naamini sisi tumejipanga kuwa na Kishapu mpya, yenye maendeleo mapya,” alieleza Khamis.

Kwa upande wake mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo hilo la Kishapu, Boniphace Butondo amekishukuru Chama chake kwa kumteua yeye kupeperusha bendera ya CCM na kwamba anaamini ataipeperusha vyema bendera hiyo kwa kukiletea ushindi chama chake.

Naye Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Emmanuel Matinyi amewataka wafuasi wote wa vyama vya siasa vitakavyosimamisha wagombea katika uchaguzi wa mwaka huu kuhakikisha vinafanya kampeni za kistaarabu zisizokuwa na aina yoyote ya vurugu ama kushambulia watu wengine.

“Tunaomba mtakapoanza kampeni kesho naomba mfanye kampeni za kistaaribu, na hasa ninyi kama chama chenye Serikali mna wajibu mkubwa wa kuonesha utii wa sheria, hasa upande wa kuzingatia ratiba zenu za kampeni, hapo ndipo penye tatizo kubwa, hivyo ikitokea mabadiliko tuarifiane mapema,” alieleza Matinyi.

Katika hatua nyingine wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wamekutana pamoja katika ofisi za Msimamizi wa uchaguzi wakati wagombea wao wa ubunge walipokuwa wakirejesha fomu za kuomba uteuzi wa kugombea Jimbo la Kishapu.

Hata hivyo wafuasi wa vyama vyote viwili walionesha hali ya furaha na hapakutokea aina yoyote ya kurushiana maneno mbali ya upande wa CCM kudai wenzao baada ya kuwaona walisalimu amri kwa kukaa kimya wakiangalia shamra shamra zilizokuwa zikifanywa na wafuasi wa CCM ambao hata hivyo waliamua kukaa pembeni ili kutoa nafasi ya wenzao wa CHADEMA kuweza kuondoka katika eneo hilo.

Msimamizi wa uchaguzi katika Jimbo la Kishapu, mkoani Shinyanga, Emmanuel Matinyi amewatangaza wagombea wa CCM, Boniface Butondo na Idd Salum wa CHADEMA kuwa wagombea wa Jimbo hilo ambapo mgombea wa NCCR – Mageuzi, Zacharia Lugwila ambaye hata hivyo mpaka jana mchana alikuwa hajarejesha fomu zake.
Kushoto ni Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Kishapu, Boniphace Nyangindu Butondo akirejesha fomu zake kwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Emmanuel Matinyi. Picha na Suzy Luhende - Kishapu
Mgombea ubunge Boniphace Butondo akisaini baada ya kukabidhi fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Kishapu kwa Msimamizi wa uchaguzi Emmanuel Matinyi
Mgombea ubunge kupitia chama Cha Mapinduzi CCM Boniphace Butondo akisalimiana na wananchi wakati akirejesha fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga
Mgombea ubunge kupitia chama Cha Mapinduzi CCM Boniphace Butondo akisalimiana na wananchi wakati akirejesha fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga

Wafuasi wa chama Cha Mapinduzi CCM wilayani Kishapu wakimsindikiza mgombea wa ubunge kupitia CCM Boniphace Butondo akirudisha fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527