WAZIRI LUKUVI APOKEA MSAADA WA COMPYUTA 10 KUTOKA BENKI YA AZANIA

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepokea msaada wa Kompyuta 10 zenye thamani ya milioni 12 kutoka Benki ya Azania.

Msaada huo ulipokelewa leo tarehe 10 Julai 2020 katika ofisi za ardhi mkoa wa Dodoma na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Wizara akiwemo Katibu Mkuu Mary Makondo.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Waziri Lukuvi aliishukuru Benki ya Azania kwa msaada huo alioueleza kuwa utasaidia sana kwenye huduma za sekta ya ardhi hasa katika ofisi za ardhi za mikoa zilizoanzishwa hivi karibuni.

Alisema, benki ya Azania imekuwa ikiunga mkono jitihada za Wizara kusaidia vifaa na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa Benki ya Azania katika kusaidia juhudi za serikali kusogeza huduma za ardhi karibu na wananchi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, hivi sasa wizara yake baada ya kuanzisha ofisi za ardhi katika mikoa inafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha ofisi hizo zinakuwa na vifaa vya kutosha kwa lengo la kuwawezesha watendaji wa ofisi hizo kufanya kazi kwa ufanisi.

Kwa upande wake Meneja wa Benki ya Azania mkoa wa Dodoma Makalla Mbura alimueleza Waziri wa Ardhi kuwa msaada uliotolewa moja ya juhudi za benki hiyo kusaidia jitihada mbalimbali zinaziofanywa na wizara ya ardhi kwenye sekta ya ardhi.

Makalla aliongeza kwa kusema kuwa, benki hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za wizara katika masuala mbalimbali ya huduma za sekta ya ardhi kwa kutoa msaada pale unapohitajika.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527