MAAFISA MADINI WAKAZI WA MIKOA WAMKOSHA WAZIRI WA MADINI

Na Tito Mselem,WM

Waziri wa Madini, Doto Biteko amewapongeza maafisa madini wakazi wa mikoa kwa utendaji mzuri uliopelekea kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli kwa mwaka wa fedha 2019-2020 ambapo walikusanya shilingi bilioni 528.2 ikiwa ni zaidi ya lengo la shilingi bilioni 470 lililopangwa.


Amebainisha kuwa ili kuendelea kufanikiwa katika kusimamia sekta ya madini viongozi wawe tayari kujifunza na hapo ndipo watafurahia matokeo ya uongozi wao kila mmoja katika eneo lake.

Waziri Biteko ameyasema hayo Julai 25,mwaka huu jijini Arusha alipokuwa akifunga mkutano wa Katibu wa Madini, Profesa Simon Msanjila na maafisa madini wakazi wa mikoa wenye lengo la kujadili mafanikio, changamoto na namna ya kuzitatua kwenye Sekta ya Madini.

Amesema, siri ya mafanikio makubwa katika Wizara ya Madini ni pamoja na ubunifu na uzalendo wa maafisa madini wakazi wa mikoa kwenye ukusanyaji wa maduhuli na kuwataka kuendelea kusimamia shughuli za uchimbaji na biashara ya madini kwa kufuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.

“Nipende kueleza kuwa, ninatambua mchango wenu mkubwa sana kwenye ukuaji wa Sekta ya Madini, mmekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kodi mbalimbali zinalipwa serikalini, hii imesaidia sana sekta ya madini kukua,”amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Biteko amewataka maafisa madini wakazi kutatua migogoro kwa kusimamia sheria na kusisitiza kuwa wasisite kuwasilisha changamoto kwa viongozi wa Tume ya Madini pale wanapokwama.

Aidha, amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuendelea kushirikiana kwa kubadilishana uzoefu kwenye usimamizi wa shughuli za madini ili kuongeza tija kwenye utendaji kazi.

Naye Naibu Waziri Nyongo akizungumza kwenye mkutano huo amewataka maafisa madini wakazi wa mikoa kuendelea kushirikiana kwa karibu na wakuu wa mikoa, wilaya, taasisi nyingine pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi wao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameeleza kuwa kushikamana, kupambana na kupiga kazi ndio uwe msingi wa maafisa hao.

Amewataka kila mmoja kuhakikisha anatimiza lengo la makusanyo ya maduhuli kwa mwaka wa fedha 2020-2021 alilopangiwa ili wizara iweze kuvuka lengo la mwaka husika.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila mbali na kuwapongeza maafisa madini hao ameongeza kuwa, imani kwa Serikali kwa Wizara ya Madini imeongezeka mara baada ya kufanikiwa kukusanya maduhuli zaidi ya lengo lililowekwa awali.

    “Mtakumbuka mwaka jana tulisaini mkataba wa shilingi bilioni 10.6 na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuimarisha Tume ya Madini kwa kununua vifaa mbalimbali pamoja na magari ambapo zimezaa matunda, endeleeni kuchapa kazi na tupo tayari kuwasaidia muda wowote,”amesema Profesa Msanjila.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Madini, Prof. Simon Msanjila amewapongeza maafisa hao na kueleza kuwa wamesababisha wizara kuaminiwa kutokana na kukidhi vigezo baada ya kufikia malengo ya makusanyo waliyoingia na Wizara ya Fedha mwezi Aprili, 2019 aliposaini mkataba na kupewa kiasi cha bilioni 10.6 ili kuimarisha Tume ya Madini.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula amekiri kuwa mafanikio yaliyopo kwenye sekta ya madini yametokana na uaminifu uliopo kwa viongozi na watendaji wa Tume ya Madini na kuwataka maafisa hao kudumisha weledi huo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Profesa Idris Kikula aliishukuru Wizara ya Madini kwa ushirikiano mzuri kwa Tume ya Madini hali iliyopelekea tume kufanya vizuri kwenye Sekta ya Madini.

Amesema kuwa, changamoto zilizoainishwa katika mkutano husika zitaandaliwa vyema na kuwasilishwa ngazi za juu na utekelezaji wake kufanyika mara moja.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527