WAZIRI MHAGAMA ATOA MAAGIZO UJENZI WA MRADI KIWANDA CHA MACHINJIO YA KISASA WA NGURU KUKAMILIKA KWA WAKATI

Na.Mwandishi Wetu – Mvomero, Morogoro

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama ameutaka uongozi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamiii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kushirikiana na Wasimamizi wa mradi Machinjio ya kisasa ya Nguru Hills Ranch ili kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati.

Waziri Mhagama ametoa maagizo hayo jana  Juni 19, 2020 wakati akikagua maendeleo ya mradi wa kiwanda hicho kilichopo Mvomero, Mkoani Morogoro, akikagua mradi huo alieleza kuwa ni vyema kasi ya ujenzi wa kiwanda hicho ikawa sambamba na ya ujenzi wa Kiwanda cha bidhaa za Ngozi cha Karanga kinachojegwa Mkoni Kilimanjaro kwa kuwa viwanda hivyo vitakuwa vikishahabiana.

“Kiwanda hiki kikikamilika kwa wakati kitatoa fursa nyingi sana kikwemo nchi jirani na mataifa mengine yataweza kununua nyama zitakazokuwa zikizalishwa kwenye kiwanda hicho pamoja uwepo wa ngozi ambazo zitakuwa zikitumiwa na kiwanda cha Karanga kutengeza bidhaa za Ngozi, hivyo viwanda vyote viwili vitakuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi” alisema Mhagama

“Nimatumaini yangu wakandarasi na wasimamizi wa mradi huu mtahakikisha mnaondoa vikwazo vinavyowakabili katika kila hatua ya ujenzi na itakuwa vizuri mkiiga mfano wa ujenzi wa Kiwanda cha Karanga kwa kuakikisha ujenzi unafanyika usiku na mchana ili kiwanda hicho kikamilike mapema kabla mwaka huu 2020 haujaisha,” alieleza Mhagama

Aliongeza kuwa azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kukuza ajira nchini na uwepo wa kiwanda hicho utasaidia kutoa fursa ya ajira kwa wananchi.

“Kiwanda hiki kitakapo kamilika kitatoa fursa kwa wakazi ambao wanaishi karibu na kiwanda hicho kupata ajira baada ya kukamilikia na pia wafugaji waliopo karibu na kiwanda watapata fursa ya kuuza mifugo yao,” alisema Mhagama

Sambamba na hayo Waziri Mhagama amehimiza suala zima la usimamiziwa fedha katika mradi huo pamoja na kuandaliwa kwa mikakati ya uendeshaji wa kiwanda hicho akitoa mfano mpango wa unenepeshaji ng’ombe ambao utaongeza uzalishaji wa nyama bora.

Pia, amewataka wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanafuatilia ujio wa wataalamu kutoka China ambao watasimika mitambo ya kuchakata nyama, ili uzalishaji kwenye kiwanda hicho uanze haraka.

Pamoja na hayo, Waziri huyo ameupongeza Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa kuwekeza kwenye miradi yenye tija na salama yenye uhakika wa faida ya malipo ya mafao kwa wanachama wake hapo baadae.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Bw. Hosea Kashimba aliahidi kusimamia mradi huo na kutekeleza maagizo yote ambayo mheshimiwa waziri ameagiza.

“Tutahakiksha tunaandaa programu nzuri zitakazo tuwezesha kama wawekezaji wa mradi huu kufikia malengo ya Serikali ili uzalishaji katika kiwanda hiki uanze mapema,” alisema Kashimba

Mradi huo wa ujenzi wa Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills uliopo Nguru ya Ndege, Mvomero unatekelezwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Kampuni ya Busara na Eclipes.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post