TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA (THBUB) YATOA TAMKO LA KUMPONGEZA RAIS MAGUFULI

TAMKO LA THBUB KUMPONGEZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHESHIMIWA DKT. JOHN  POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA HOTUBA YA KULIFUNGA BUNGE LA 11 ALIYOITOA KATIKA UKUMBI WA BUNGE, DODOMA TAREHE 16 JUNI, 2020

Tarehe 16 Juni 2020, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa Hotuba ya Kufunga Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ukumbi wa Bunge, Dodoma. 

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inatoa pongezi za dhati kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Hotuba yake iliyojaa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano cha uongozi wake, yaani kuanzia mwaka 2015 hadi 2020. 

hiyo ilieleza kwa kina mafanikio mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kijamii yaliyopatikana katika kipindi hicho.

 Aidha, hotuba hiyo ilisheheni hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kuimarisha haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.

Mhe. Rais alieleza kuwa katika awamu ya tano uchumi wa nchi ya Tanzania umekuwa kwa asilimia 6.9 kutoka 6.2 mwaka 2015 na pato ghafi la Serikali kuongezeka kutoka milioni 345 hadi milioni 1,399 na kufanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 zenye uchumi mkubwa zaidi Barani Afrika na kwamba kiwango cha umaskini kimepungua hadi asilimia 26.4 mwaka 2020. 

THBUB imeona kwamba kwa ukuaji huu wa uchumi imewezekana kuimarisha upatikanaji wa haki mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Katika kuzingatia haki za binadamu, Mhe. Rais alielezea pamoja na mambo mengine, mafanikio katika upatikanaji wa haki ya afya, elimu na upatikanaji wa maji safi na salama. 

Aidha, Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza na kusogeza karibu na wananchi vituo vingi vya kutolea huduma za afya zikiwemo zahanati, vituo vya afya, na hospitali za Wilaya, Mikoa, Rufaa na Kanda. 

Kwa upande wa sekta ya elimu, Serikali iliendelea kutoa elimu bila ya malipo kwa shule za msingi na sekondari pamoja na kuongeza shule za msingi, sekondari, vyuo vya ufundi, kujenga mabweni, maabara na kuongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu.

Katika kuimarisha utawala bora na utoaji haki, Serikali ya Awamu ya Tano iliteuwa majaji 17 wa Mahakama ya Rufani na 52 wa Mahakama Kuu na kuajiri watumishi wengine 890 wa mahakama, wakiwemo Mahakimu 396. Aidha, Serikali ilijenga Mahakama Kuu mbili, Mahakama za Hakimu Mkazi tano, Mahakama za Wilaya 15 na Mahakama za Mwanzo 18. 

Hatua hizi zimesaidia kuharakisha usikilizwaji wa mashauri na hivyo kusaidia kupatikana kwa haki kwa wakati. Katika kipindi cha miaka mitano Serikali ilipunguza mlundikano wa mahabusu ambapo mahabusu wapatao 2,812 wamefutiwa kesi zilizokuwa zinawakabili. Aidha, Mhe. Rais alitoa msamaha kwa wafungwa  42,774.

Pia, Serikali ya Awamu ya Tano iliimarisha maadili na nidhamu ya kazi nchini ambapo jumla ya watumishi 32,555 walichukuliwa hatua mbalimbali zikiwemo kuwashusha vyeo, kuwapunguzia mishahara na kuwapa onyo kali. 

Vile vile, watumishi 15,508 walifukuzwa kazi kwa kukutwa na vyeti feki na idadi ya ajira hewa 19,708 zilibainika ambazo zilikuwa zikiigharimu Serikali T.Shs. Bilioni 198 kila mwezi. Katika kupambana na rushwa, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imeweza kufungua mashauri 2,256, ambapo mashauri 1,926 tayari yametolewa uamuzi.

Katika kulinda haki na demokrasia nchini, Mhe. Rais kwa mara nyingine ameirejea ahadi yake aliyoitoa katika sherehe za Maadhimisho ya Muungano zilizofanyika jijini Mwanza tarehe 26 Aprili, 2020, amewahakikishia Watanzania kuwa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 utakuwa huru na wa haki. 

Sambamba na ahadi hiyo, Mhe. Rais amevitaka vyama vya siasa na wanasiasa kujiandaa ili kushiriki kikamilifu katika uchaguzi na kujiepusha na matusi, kejeli na kumtanguliza Mungu katika kampeni za uchaguzi.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inawaomba Watanzania kuendelea kulinda na kuthamini hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kulinda haki za binadamu na kudumisha amani na utulivu uliopo pamoja na kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora ambavyo ni chachu ya amani na utulivu wa Taifa letu.

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa mara nyingine inampongeza sana Mhe. Rais kwa kutoa matumaini makubwa kwa wananchi katika kuendelea kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora nchini.

Imetolewa na:

(SIGNED)
Mathew Pauwa Mhina Mwaimu (Jaji Mstaafu)
Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Juni 19, 2020


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527