MTENDAJI AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUPAPASA MATITI YA MTOTO


Mtendaji wa Mtaa wa Kyakailabwa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba akikabiliwa na mashtaka mawili ya kumtorosha mtoto mwenye umri wa miaka 14 na kumfanyia shambulio la aibu la kumpapasa matiti.

Kesi hiyo namba 149 ya mwaka 2020, imesomwa Mahakamani hapo na Wakili wa Serikali Joseph Mwakasege, mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo Ruth Migan, amesema mshtakiwa huyo Patrick Rwegasira mwenye umri wa miaka 44 baada ya kumtorosha mtoto huyo, aliishi naye kwake na alimpapasa matiti akilenga kumfanyia vitendo vya aibu.

Mwakasege amesema kuwa mshtakiwa huyo alimchukua mtoto huyo kutoka kwa wazazi wake Juni 2 hadi 04 mwaka huu alipokamatwa na kupelekwa Polisi.

Akijitetea mshtakiwa huyo amedai kuwa mtoto huyo hajamtorosha, bali alikutana naye mtaani baada ya kufukuzwa na wazazi na kuamua kumpa hifadhi kama Mtendaji.

Mshtakiwa amerejeshwa rumande kutokana na kukosa wadhamini na kesi yake itatajwa tena Julai 6 mwaka huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527