RAIS MAGUFULI ATAKA ANAOWATEUA WARIDHIKE: “KAMA UNA UHAKIKA UKIENDA KULE UTASHINDA....NENDA KWA SPIDI KUBWA”


Rais wa Tanzania John Magufuli amewaasa viongozi anaowateua kuridhika na nafasi wanazopatiwa akisema kuwa haiwezekani ukapata kila kitu.

Magufuli ameyasema hayo alipokuwa akiwaapisha Bw. Idd Hassan Kimanta kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, katika hafla iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam na kuapa kwa viongozi wengine walioteuliwa wa Mkoa wa Arusha, Kamishna wa polisi Edward Jotham Balele kuwa Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Bw.Kenan Laban Kihongosi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

''Niendelee kutoa wito kwa viongozi ninaowateua wajifunze pia kuridhika na nafasi walizonazo, nitashangaa sana kama IGP ataondoka hapa aende akagombee Bunda, kwa sababu anatoka Bunda, akawa anaomba ubunge akitegemea nitamteua kuwa waziri, kwanza hana uhakika kama atashinda katika kura za maoni na anawezekana akashinda na bado nikamfuta.'' Alieleza Rais Magufuli

''Ni kuridhika lakini hauwezi kuwa na kila kitu, lakini Demokrasia iko huru kama una uhakika kabisa kuwa ukienda kule utashinda tu, basi nenda tu, nenda tena nenda kwa spidi kubwa, lakini mimi ninafikiri saa nyingine ni kuridhika, kila mahali unaweza kufanya maajabu katika position yako, vinginevyo huwezi kuwa na kila kitu, inawezekana huwezi ukawa na kila kitu.'' Alisema.

Rais Magufuli ameeleza sababu za kutengua uteuzi wa viongozi watatu wa Mkoa wa Arusha kuwa ni kutokana na viongozi hao kutoelewana na kugombana bila sababu za msingi licha ya kuonywa mara kadhaa, na ametaka vitendo hivyo visijirudie kwa wateule wapya na viongozi wengine nchini.

''Mimi saa nyingine huwa nasikitika sana unapowaona watu uliowateua na kuwaapisha na kuwaamini kwa niaba ya watanzania wanapokwenda kule hawafanyi kadiri ya viapo walivyonavyo.''

''Mtakumbuka hivi karibuni Arusha ilibidi nitengue uteuzi wa wote niliokuwa nimewateua kuanzia RC, Mkurugenzi wa mji pamoja na DC ni kwasababu katika kipindi cha miaka karibu miwili walikuwa wanagombana tu, kila mmoja ni bosi kila mmoja anatengeneza mizengwe dhidi ya mwenzake... Sikufurahishwa''.''Walifanya kazi zao lakini waliniudhi wao kutokushirikiana kufanya yale ambayo nimewaagiza,

''Sasa nimewateua ninyi sitaki yajitokeze hayo, kafanyeni kazi na mkaridhike na mlicho nacho kwasababu ...tatizo jingine la vijana unapompa nafasi wana tabia ya kutoridhika na hizo nafasi wanashindwa kujua kuwa miaka bado ipo mingi sana, sasa mkaridhike na kazi mliyonayo mkawatumikie watanzania''.

Kuhusu migogoro inayoabili Arusha , Magufuli amewataka viongozi kusimamia sheria na kuzingatia viapo vya maadili ya kazi wakati wa utekelezaji wa majukumu mbali mbali.

''Kwa sababu RPC yupo hapa, IGP yupo hapa yule wa TAKUKURU yuko hapa, mkawaonye watendaji wenu walioko Arusha.. wakafanye kazi nilizowatuma wasifanye kazi ambazo sikuwatuma,nao leo nilikuwa niwatoe RPC pamoja na mkuu wa TAKUKURU wa Arusha lakini nimeona niwaonye hapahapa, nimeamua kuwasamehe lakini sijawasemehe moja kwa moja, wakifanya kosa lolote wataondoka nataka wakafanye kazi nilizowatuma sio kazi wanazojituma wao.''

''Nimejitahidi sana kuwasamehe kwa sababu haiwezekani ukawa umewatuma watu kwenda kufanya kazi za serikali wanakwenda kufanya shughuli zao, nyinyi mnafahamu shughuli walizokuwa wanazifanya hasa katika kipindi hiki kifupi. Kwa hiyo kawafikishie ujumbe.'' Alisema Magufuli

Rais Magufuli amemtaka mkuu mpya wa mkoa kusimamia migogoro mkoani Arusha ambayo amedai kuwa mingine ilikuwa ikitengenezwa kwa makusudi kama vile mgogoro wa kanisa na shule. Mgogoro ambao ulishamalizwa zamani kuwa kama shule inahitaji eneo zaidi ijenge ghorofa katika shule yao.

''Palikuwa na mgogoro kwa waislamu , eneo la msikiti ni mita za mraba 10495 na eneo la wazi ni mita 4165, kuna kiongozi mmoja alikuwa akihubiri kwa ndugu zetu waislamu, ombeni na hii open space, Mkurugenzi alipokataa, ikawa Mkurugenzi amekataa kutoa eneo, ni kuchonganisha uongozi wa mkurugenzi na ndugu zetu waislamu''.

Lakini tatizo lile limesababishwa na Mkuu wa Mkoa, anazungumza hivi huku, na huku anazungumza hivi huku, lengo ni kuonekana kwamba yeye ni mzuri sana, kila mmoja anatoa ahadi, tusitoe ahadi ambazo haziwezekani ni lazima tusimamie sheria.''

''Na hili liwe fundisho kwa viongozi ninaowateua, lazima mkajenge element za kuvumiliana, lazima tujifunze kuzingatia sheria na maadili na viapo vyetu tunavyoviapa.'' Alieleza Rais Magufuli.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527