Breaking : RAIS MAGUFULI ATANGAZA SHULE ZOTE,SHUGHULI ZOTE ZIFUNGULIWE TANZANIA KUANZIA JUNI 29Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Dk. John Magufuli ametangaza rasmi kuwa Juni 29,2020 shule zote ambazo zilikuwa zimefungwa kwa sababu ya ugonjwa wa Corona zifunguliwe huku akitangaza kurejesha shughuli zote za kijamii na kimaendeleo ambazo nazo zilisimama kwani ni lazima maisha mengine lazima yaendelee.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 16, 2020 wakati akilihutubia na kulifunga Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma ambalo limemaliza muda wake rasmi leo.

Amesema hivi sasa nchini Tanzania maambukizi ya Virusi vya Corona yamepungua sana na hivyo shule zote ambazo zilikuwa zimefungwa zifuguliwe rasmi Juni 29 mwaka huu.

"Juni 29,2020 shule zote ambazo zilikuwa zimefungwa kwa sababu ya Corona zifunguliwe. Pia shughuli zote ambazo zilikuwa zimesimama kupisha janga hilo nazo tunaruhusu zianze kuanzia tarehe hiyo, maisha lazima yaendelee.Nawashukuru Watanzania wote kwa kushinda vita dhidi ya mapambano ya Corona,"amesema Rais Magufuli.

"Siku zote njia ya kukabiliana na changamoto ni kukabiliana nayo, ndio maana tuliamua kukabiliana na Corona kwa kumtanguliza Mungu na mpaka sasa tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa.Sio tu kufanikiwa kuushinda ugonjwa huo bali pia kushinda athari zake iwemo ya kiuchumi.

"Kwa hiyo nitumie fursa hii kurudia kumshukuru Mungu kwa kutuepusha na Corona lakini pia tunawashukuru viongozi wetu wa dini kuitikia mwito wa Serikali wa kufanya maombi.Najua kwenye Mungu hakuna kinachoshindikana,"amesema Rais Magufuli.

Pia emewapongeza madaktari kwa kazi nzuri, amewapongeza Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia ,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu kwa ujasiri mkubwa ambao ameuonesha wakati wa janga la Corona.

"Nataka kusema kwa dhati nimemtesa mama huyu, nilikuwa nampiga simu hadi saa nane usiku.Naomba aniombee msamaha kwa mumewe. Namshukuru Waziri Mkuu na Kamati yake, nawashukuru Kamati ya Ulinzi na Usalama, nawashukuru Watanzania kwa kumtanguliza Mungu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post