HUHESO FOUNDATION YATOA MSAADA WA VIFAA VYA KUJIKINGA NA CORONA KAHAMA


Shirika la Huheso Foundation lenye makao yake Malunga Wilayani Kahama mkoani Shinyanga limetoa msaada wa vifaa vya kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne katika halmashauri ya Mji wa Kahama.

Akikabidhi vifaa hivyo leo Jumatatu Juni 1,2020 kwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha, Mkurugenzi wa shirika la Huheso Foundation na Huheso Fm Radio Bw. Juma Mwesigwa amesema vifaa hivyo ni kwa ajili ya kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali katika mapambano dhidi ya virusi vya Corona.

Mwesigwa amevitaja vifaa hivyo vilivyotolewa kwa halmashauri ya Mji wa Kahama kuwa ni ndoo 40, vitakasa mikono lita 10, sabuni za kunawia Boksi 8 na barakoa 150.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha amelishukuru shirika la Huheso Foundation kwa kutoa msaada huo hasa kipindi hiki cha mapambano ya virusi vya Corona.

Macha amesema msaada huo umekuja wakati muafaka ambapo leo shule zenye wanafunzi wa kidato cha tano zimefunguliwa hivyo msaada huo utasaidia katika maeneo hayo baada ya ofisi ya Mganga Mkuu kuviratibu vifaa hivyo.

Hata hivyo amesema kuwa serikali imejitahidi kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kwa wananchi na ugonjwa huu wa Covid 19 umepungua hapa nchini hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kumuomba Mungu sambamba na kufuata maelekezo yote yanayotolewa na Serikali ikiwemo kuchukua tahadhari zote ili wasipate maambukizi ya virusi vya Corona.

Aidha shirika la Huheso limetoa msaada huo baada ya kupata ufadhili wa mradi wa Baki Salama wenye lengo la kuwajengea uwezo kamati ya afya ya wilaya, sambamba na kamati ya MTAKUWWA kwa kuangalia kuwa kutokana na ugonjwa wa Covid -19 kundi la wanawake na watoto ni athari gani zinajitokeza katika kundi la wanawake pamoja na watoto.

Mradi huo wa Baki salama unafadhiliwa na The Foundation for Civil Society na unatekelezwa katika kata tano za Zongomela, Kahama mji, Majengo, Nyasubi na Malunga lengo likiwa ni kutoa elimu kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ili wasiweze kupata maambukizi ya virusi vya Corona.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha (aliyevaa suti) akiangalia vifaa vya kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne  vilivyotolewa Shirika la Huheso Foundation.

Kulia ni Mkurugenzi wa shirika la Huheso Foundation na Huheso Fm Radio Bw. Juma Mwesigwa  akimkabidhi Sanitizer Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha ikiwa ni sehemu vifaa vya kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne vilivyotolewa na shirika hilo.

Kulia ni Mkurugenzi wa shirika la Huheso Foundation na Huheso Fm Radio Bw. Juma Mwesigwa  akimkabidhi ndoo Mkuu wa wilaya ya Kahama Anamringi Macha ikiwa ni sehemu vifaa vya kujikinga na Maambukizi ya virusi vya Corona vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni nne vilivyotolewa na shirika hilo.

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527