GARI LA HALMASHAURI YA USHETU LAPATA AJALI..DEREVA AFARIKI DUNIA, AFISA KILIMO MAPENZI AJERUHIWA


Muonekano wa Gari lenye namba za usajili SM 12482 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya halmashauri ya Ushetu baada ya kupata ajali Mjini Kahama -Picha na Shaban Njia - Kahama

   Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Dereva wa gari la halmashauri ya Ushetu wilaya ya Kahama mkoa wa Shinyanga Stanslaus Njau (45) amefariki dunia huku Afisa Kilimo wa halmashauri ya Ushetu,Mapenzi Wilson Mshana (53) akijeruhiwa baada ya gari hilo lenye namba za usajili SM 12482 aina ya Toyota Land Cruiser kuacha njia na kupinduka. 


Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Debora Magiligimba ajali hiyo imetokea jana Jumapili Mei 31,2020 majira ya saa tatu na dakika ishirini usiku katika eneo la D4N Mbulu, barabara ya Kahama - Isaka, Kahama Mjini. 

“Gari lenye namba za usajili SM 12482 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya halmashauri ya Ushetu likiendeshwa na Stanlaus Njau (45), dereva mkazi wa Mhungula likiwa linatokea Kagongwa kuelekea Kahama Mjini liliacha njia, kupinduka na kusababisha kifo kwa dereva wa gari hilo”,amesema Kamanda Magiligimba. 

“Gari hilo pia lilisababisha majeruhi kwa Mapenzi Wilson Mshana (53) ambaye ni Afisa Kilimo wa halmashauri ya Ushetu na mkazi wa Majengo Kahama ambaye amepata majeraha sehemu ya mguu wa kushoto”,ameeleza Kamanda Magiligimba. 

Amesema gari husika lipo kituo cha polisi Kahama na majeruhi amelazwa katika haspitali ya halmashauri Mji wa Kahama akiendelea na matibabu na hali yake inaendelea nzuri. 

Kamanda Magiligimba amekitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendokasi na kwamba mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo ukisubiri ndugu kwa taratibu za mazishi. 


Kamanda Magiligimba anatoa wito kwa madereva kufuata sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali barabarani.


Muonekano wa Gari lenye namba za usajili SM 12482 aina ya Toyota Land Cruiser mali ya halmashauri ya Ushetu baada ya kupata ajali Mjini Kahama na kusababisha kifo cha dereva wa gari  Stanslaus Njau (45) na kujeruhi Afisa Kilimo wa halmashauri ya Ushetu,Mapenzi Wilson Mshana (53). Picha zote na Shaban Njia - Kahama


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527