MAWAZIRI 10 WAAMBUKIZWA CORONA SUDAN KUSINI


Mawaziri 10 wameambukizwa virusi vya corona nchini Sudan Kusini, msemaji wa serikali ameithibitishia BBC. 


Waziri wa Habari wa Sudani Kusini Michael Makuei ameiambia BBC kuwa mawaziri wote hao walikuwa ni wajumbe wa kamati ya juu ya serikali ya kupambana na corona nchini humo.

Katika mawaziri waliopo kwenye kamati hiyo, ni Waziri wa Afya pekee ambaye hajakutwa na maambukizi.

Inaripotiwa kuwa mawaziri hao wamepata maambukizo baada ya kukutana na aliyekuwa mjumbe wa kamati hiyo ambaye alikuwa na virusi vya corona.

Mawaziri wote 10 wamejitenga kwa sasa na serikali imesema kuwa wote wanaendelea vizuri kiafya.

Taarifa za kuambukizwa kwa mawaziri hao zinakuja siku chache baada ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa nchi hiyo Riek Machar kutangaza kuwa amekutwa na virusi pamoja na mkewe, ambaye ni Waziri wa Ulinzi.

Walinzi wa viongozi kadhaa nchini humo wamekutwa na virusi na kwa sasa wapo karantini.

Mpaka sasa zaidi ya watu 300 wamethibitishwa kupata corona Sudani Kusini, huku watu wane wakipona na sita kufariki.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527