PROFESA ALIYEKUWA ANAFANYA UTAFITI KUHUSU VIRUSI VYA CORONA AUAWA KWA KUPIGWA RISASI MAREKANI

Mauaji ya raia wa China, mtafiti wa masuala ya virusi vya corona kwenye ardhi ya Marekani yamesababisha nadharia mbalimbali duaniani kuwa kuna sababu iliyojificha kuhusu kifo chake.

Bing Liu, profesa msaidizi mwenye miaka 37 katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Pittsburgh, Marekani alipatikana akiwa amekufa nyumbani kwake siku ya Jumamosi.

Wenzake walisema alikuwa karibu kupata "matokeo muhimu" ya tafiti kuhusu Covid-19, tukio lililosababisha kuwepo kwa maoni mitandaoni yanayoeleza kuwa yawezekana bwana Liu aliuawa lakini polisi wanasema ni tukio la kujiua.

Kwa nini Liu aliuawa?

Alikutwa akiwa na majeraha mengi ya risasi kichwani,shingoni katika eneo la Pittsburgh yalipo makazi yake kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo.

Mtu aliyekuwa na silaha alitambulika kuwa na miaka 46, mhandisi wa programu ya kompyuta, Hao Gu. Mamlaka zinasema muuaji naye alijiua baada ya kurudi kwenye gari lake.

Liu na Gu walikuwa wanafahamiana, maafisa wapelelezi wa mauaji walieleza.

Uchunguzi umebaini kuwa lilikuwa tukio la kuua na kujiua lililotokana na ''mgogoro wa muda mrefu wa masuala ya kimapenzi''.

Wamesema ''hakuna ushahidi'' wa kuhusisha tukio hilo na utafiti wa Liu na mazingira ya sasa ya changamoto za kiafya.
Liu ni nani?

Katika taarifa yao , wenzake wamemwelezea kama mtafiti wa kipekee ambaye ''alikuwa ukingoni kufanikisha kupata matokeo muhimu '' ya kuelewa maambukizi ya Covid-19.

Waliomboleza kifo cha Liu na kuahidi kumalizia utafiti wake ''zikiwa ni juhudi za kuenzi ubora wake katika uwanja wa kisanyansi''.

Liu, raia wa China alipata shahada yake ya kwanza na shahada ya uzamivu katika masomo ya sayansi ya kompyuta nchini Singapore kabla ya kufanya utafiti nchini Marekani.

Aliwahi kuungana na wanabaiolojia wengine kufanya utafiti kuhusu kinga ya binaadamu, kwa mujibu wa wasifu wake mtandaoni.

Yanayozungumzwa mitandaoni.

''Mungu wangu'' mtumiaji mmoja wa mtandao wa kijamii wa Weibo aliandika. '' Labda alibaini kuwa virusi vilitengenezwa kwenye maabara nchini Marekani.''

Maoni kama hayo yalieleza kuwa Liu aliuawa kwa sababu pengine aligundua chanzo cha virusi vya corona.

Maafisa wa China na vyombo vya habari vya habari vya serikali vilisema kuwa madai yakuwa virusi vilitengenezwa Marekani na kupelekwa Wuhan na wanajeshi wa Marekani hayana msingi.

Wengine walisema ni tukio ambalo lina sababu iliyojificha.

''Inawezekana kuwa kuna siri iliyojificha gizani''. Alieleza mtu mmoja kwenye mtandao huo.

Maoni mengi ya watu kwenye mtandao huo yanasema kuwa historia ya Liu inaweza kuwa ndio iliyomuweka hatarini nchini Marekani, ingawa hakuna ushahidi ulioibuka kuwa Liu alikuwa akilengwa kwa sababu ya asili yake.

Gazeti ka Global Times linalofungamana na chombo cha habari cha taifa nchini china, lilichapisha makala kuhusu mazingira ya kifo cha Liu.

Kwenye mtandao wa Twitter, baadhi wameeleza hisia zao kuwa huenda serikali ya China ina mkono wake kwenye tukio hilo.

Kutokana na janga la Covid-19, nadharia mbalimbali kuhusu virusi na asili yake zimeendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii.

Nyingine zikiwa na madai yasiyothibitishwa zimekuwa zikiungwa mkono na wanasiasa na vyombo vya habari vya China na Marekani.
CHANZO - BBC SWAHILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527