MASHITAKA MAWILI YANAYOWAKABILI IDRIS SULTAN NA MWENZAKE


Msanii wa vichekesho, Idris Sultan, na mwenzake, Innocent Maiga wamefikishwa katika Mahakama ya Kisutu leo Mei 27, 2020, na kusomewa mashtaka yanayowakabili likiwemo la kumiliki laini ya simu ya Maiga na kushindwa kuripoti mabadiliko ya umiliki wa laini hiyo.

Washitakiwa wamesomewa mashitaka yao na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Matilda Mushi na Estazia Wilson mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rashid Chaungu. Kosa la kwanza la kushindwa kufanya usajili wa simu wa kadi iliyokuwa inamilikiwa na mtu mwingine linamkabili Idris Sultan.

Katika kesi hiyo ya jinai, inadaiwa ametenda kosa hilo kati ya Desemba 1, 2019 na Mei 19, 2020, maeneo ya Mbezi Beach Kinondoni ambapo alitumia kadi ya simu iliyomilikiwa na Innocent Maiga bila kuripoti kwa mtoa leseni.

Kosa jingine ni kushindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya kadi ya simu ambapo linamkabili Innocent Maiga ambaye anadaiwa amelitenda Desemba 1, 2019 na Mei 19, 2020 Mbezi Beach Kinondoni ambapo ni kinyume na sheria kwani alishindwa kutoa taarifa ya mabadiliko ya namba ya simu kama inatumiwa na Idris Sultan.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, washitakiwa walikana makosa yao, ambapo upelelezi wa kesi hiyo umekamilika. Hata hivyo, washitakiwa hao wameachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh. mil. 15 kila mmoja.

Hata hivyo, Wakili wa Idris Sultan, Benedict Ishabakaki, ameondolewa kumwakilisha mshitakiwa huyo kwa sababu atatumika kama sehemu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri kutokana na kushuhudia mshitakiwa wake akichukuliwa maelezo polisi, hivyo anabakia wakili mmoja ambaye ni Jebrah Kambole.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527