HOTUBA YA BAJETI WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO MWAKA 2020/21


MAELEZO YA MHESHIMIWA DKT. PHILIP I. MPANGO (MB.), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO WAKATI AKIWASILISHA BUNGENI HOTUBA YA MAKADIRIO YA MAPATO NA
MATUMIZI YA WIZARA YA FEDHA NAMIPANGO
 KWA MWAKA 2020/21


1.0              TANGULIZI

1.          Mheshimiwa Spika,  kutokana na taarifa iliyowasilishwa ndani ya Bunge lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, iliyochambua bajeti za mafungu  ya Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi  kwa mwaka 2020/21, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka 2019/20 na  kuidhinisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya mafungu saba (7) ya Wizara pamoja na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzikwa mwaka 2020/21.

2.          Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kutujalia afya njema pamoja na kutuwezesha kuendelea kutekeleza majukumu yetu kwa Taifa na leo amenipa kibali kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuwasilisha Mpango na Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka ujao wa fedha.

3.          Mheshimiwa Spika, kwa moyo wa dhati kabisa, napenda kutoa shukrani zangu kwa kiongozi wetu, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuniamini kusimamia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kipindi chote cha muhula wa kwanza wa Serikali yake. Ni heshima kubwa kwangu kufanya kazi chini ya Kiongozi Mkuu wa nchi huyu ambaye ana upeo mkubwa sana, mchapa kazi, mwenye uzalendo wa kweli na ambaye ameistaajabisha dunia kwa kutekeleza mambo makubwa ya kimaendeleo kwa kipindi kifupi. Itoshe tu kusema namshukuru sana, naendelea kumuombea afya njema yeye na familia yake ili kazi kubwa aliyoianza ya kuwaletea maendeleo  makubwa wananchi wa Tanzania iweze kukamilika. Ahadi yangu kwa Mheshimiwa Rais na Watanzania ni kuwa, nitaendelea kuchapa kazi katika kipindi chote cha utumishi wangu ili kuenzi nafasi hii adhimu niliyokabidhiwa ya kutoa mchango wangu kwa mama Tanzania.  

4.          Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda nitumie jukwaa hili kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kabisa, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Kassim M. Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna walivyojitoa katika kuwahudumia Watanzania. Nimefurahi kufanya kazi chini yao na ninawasihi Watanzania kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia wasaidizi hawa waandamizi wa Mheshimiwa Rais ambao ni makini na wenye mapenzi ya dhati kwa nchi yao. Tuendelee kwa pamoja kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu ili waendelee  kuwa na afya njema na pia hekima na busara katika kazi zao za kumsaidia Kiongozi Mkuu wa Nchi.

5.          Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi, kwa kusimamia mhimili huu wa Bunge kwa umahiri mkubwa sana. Aidha, ninakupongeza pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa kuongoza vyema majadiliano ya Bajeti za Wizara mbalimbali. Naomba pia nitumie fursa hii kuishukuru kipekee Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Mashimba Mashauri Ndaki (Mb.), kwa maoni, ushauri na mapendekezo mazuri waliyotupatia wakati wa kuchambua mapendekezo ya Bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2020/21. Nakiri kwamba mimi binafsi, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.), Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara yetu na taasisi zake tumejifunza mambo mengi mazuri kutokana na hoja na ushauri wa Kamati hii nyeti. Vile vile, napenda nitumie fursa hii, kuwapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri wote wa Serikali ya Awamu ya Tano kwa kusimamia majukumu ya Wizara zao vizuri na kupelekea kupatikana kwa mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2015 - 2020.

6.          Mheshimiwa Spika, naomba nitumie pia nafasi hii kumpongeza sana Comred Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb.) kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria. Aidha, natoa pole kwa Bunge lako Tukufu kwa kumpoteza Mhe. Balozi Dkt. Augustine Philip Mahiga aliyekuwa Mbunge wa Kuteuliwa - CCM na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Rashid Ajali Akbar, aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini-CCM, Mhe. Mchungaji Dkt. Getrude Pangalile Rwakatare, aliyekuwa Mbunge Viti Maalum – CCM na Mhe. Richard Mganga Ndassa (Senator) aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Sumve-CCM. Tunawaombea ili wapate rehema kwa Mungu, wapumzike kwa amani. Amina.

7.          MheshimiwaSpika, namshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge makini wa Kondoa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, kwa msaada mkubwa anaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Nampongeza sana kwa uchapakazi na kujitoa kwake na napenda niwaombe Wananchi wa Jimbo la Kondoa wamrejeshe kwa kishindo mama huyu Hodari katika Bunge lijalo. Aidha, nawashukuru sana watumishi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Doto M. James, Naibu Makatibu Wakuu Bi. Amina Kh. Shaaban, Bw. Adolf H. Ndunguru na Bi. Mary N. Maganga kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Vile vile, nawashukuru Wakuu wa Mashirika na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango (CAG, BOT, TRA, NBS, TR, TRAT, TRAB, Benki  za Serikali, Taasisi 5 za mafunzo ya Elimu ya Juu na Bodi za Kitaaluma na Kitaalam) pamoja na watumishi wote wa taasisi hizo kwa ushirikiano walionipatia katika kipindi chote cha utumishi wangu kama Waziri wa Fedha na Mipango.

8.          Mheshimiwa Spika, naomba sasa nijielekeze kwenye hoja yangu. Nitaanza kwa kuelezea mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya Wizara kwa mwaka 2019/20, maeneo ya kipaumbele pamoja na mikakati mbalimbali ambayo itatekelezwa na Wizara kwa mwaka 2020/21. Aidha, nitawasilisha Mpango na Bajeti ya mwaka 2020/21 kwa mafungu saba (7) ya Wizara ambayo ni Fungu 7 – Ofisi ya Msajili wa Hazina, Fungu 10 – Tume ya Pamoja ya Fedha, Fungu 13 – Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu, Fungu 21 – HAZINA, Fungu 22 – Deni la Taifa na Huduma Nyingine, Fungu 23 – Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali na Fungu 50 – Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Fungu 45 - Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi.

2.0.     MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA 2019/20 NA MALENGO YA MWAKA 2020/21

Mapitio ya Mapato na Matumizi

9.          Mheshimiwa Spika,mapitio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni kama inavyooneshwa katika hotuba yangu kuanzia ukurasa wa 5 hadi ukurasa wa  8.

Utekelezaji wa Majukumu kwa mwaka 2019/20 na Mpango wa Mwaka 2020/21


10.      Mheshimiwa Spika, naomba kulielekeza Bunge lako Tukufu kwa ufupi juu ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa kipindi cha kuanzia Julai 2019 hadi Machi 2020 pamoja na Mpango na Bajeti ya mwaka 2020/21. Maelezo ya kina yapo katika hotuba yangu ukurasa wa 8 hadi wa 33.

(i)            Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera za Uchumi Jumla


11.      Mheshimiwa Spika, Pato la Taifa limekua kwa asilimia 7.0 mwaka 2019, kama ilivyokuwa mwaka 2018. Sekta zilizoongoza katika ukuaji ni pamoja na Uchimbaji wa Madini na Mawe asilimia 17.7, Ujenzi asilimia 14.1, Sanaa na Burudani asilimia 11.2 na Usafirishaji na Uhifadhi wa Mizigo asilimia 8.7. Sekta zilizokuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa kwa mwaka 2019 ni: Kilimo (asilimia 26.6); Ujenzi (asilimia 14.3); Biashara na Matengenezo (asilimia 8.8); Viwanda (asilimia 8.5) na Usafirishaji na Uhifadhi mizigo (asilimia 6.9). Aidha, mfumuko wa bei umeendelea kubaki katika wigo wa tarakimu moja ambapo kwa mwezi Machi 2020, ulikuwa asilimia 3.4.

12.      Mheshimiwa Spika, kutokana na uchambuzi wa awali, shabaha za uchumi jumla katika mwaka 2020/21 ni kama ifuatavyo: Pato halisi la Taifa linatarajiwa kukua kwa asilimia 4.0 mwaka 2020; mfumuko wa bei kubaki katika wigo wa tarakimu moja; nakisi ya bajeti ya Serikali kufikia asilimia 2.8; mapato ya ndani asilimia 14.5 ya Pato la Taifa; na mapato ya kodi asilimia 12.5 ya Pato la Taifa. Matarajio haya yanatarajiwa kupungua kutegemea ukubwa wa athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu (unaosababishwa na Virusi vya CORONA) kwenye sekta mbalimbali.

(ii)          Uandaaji, Utekelezaji na Usimamizi wa Mikakati, Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Bajeti ya Serikali


13.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Wizara  ilifanikiwa kuandaa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21; kuandaa taarifa ya Hiari ya Nchi Kuhusu Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 (SDGs); kuunda mfumo wa kitaasisi wa ufuatiliaji na utoaji wa taarifa za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 pamoja na mfumo wa awali (prototype) wa Kanzidata ya Kuhifadhi na Kutoa Taarifa za Miradi ya Maendeleo.

14.      Mheshimiwa  Spika, Wizara imechukua hatua za kimkakati za kuimarisha ukusanyaji wa mapato kama zinavyoonekana katika hotuba yangu ukurasa wa 11 hadi wa 14. Hatua hizo zimeiwezesha Serikali kukusanya mapato ya ndani ya jumla ya shilingi trilioni 16.06 katika kipindi cha Julai 2019 hadi Machi 2020, sawa na asilimia 92.4 ya lengo. Mapato ya ndani yameongezeka kutoka shilingi trilioni 14.07 hadi shilingi trilioni 16.06, sawa na asilimia 14.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2018/19.

15.      Mheshimiwa Spika, kati ya Julai 2019 na Machi 2020, Wizara imefanikisha upatikanaji wa fedha za misaada na mikopo nafuu ya jumla ya shilingi trilioni 2.04 sawa na asilimia 93 ya lengo la kipindi hicho la shilingi trilioni 2.78. Aidha, Wizara imefanikisha mkopo wa kiasi cha shilingi trilioni 3.44 kutoka katika soko la ndani, sawa na asilimia 101.5 ya lengo la kukopa shilingi trilioni 3.39 namkopo wa shilingi trilioni 1.82kutoka soko la nje sawa na asilimia 78.66 ya lengo la kukopa shilingi trilioni 2.32.

16.      Mheshimiwa Spika,hadi kufikia mwezi Machi 2020, jumla ya shilingi trilioni 24.65 zilitolewakwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 1.16 zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kielelezo na shilingi bilioni 597.54 kwa ajili ya kulipa madai yaliyohakikiwa. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 33.98sawa na asilimia 84.95 ya bajeti iliyotengwa zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 18 ya kimkakati inayotekelezwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

(iii)         Kubuni, Kuunda na Kusimamia Mifumo ya Usimamizi wa Fedha na Mali za Umma


17.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeboresha Mfumo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (GePG) kwa kuongeza huduma kwa njia ya simu za kiganjani (GePG application mobile) na kwa kuunganisha mfumo huo na mifumo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ya ukusanyaji wa mapato. Utekelezaji wa jukumu la kubuni, kuunda na kusimamia mifumo ya usimamizi wa fedha na mali za umma umefafanuliwa kwa kina katika hotuba yangu ukurasa wa  14 hadi wa 15.


(iv)        Usimamizi wa Sekta ya Fedha 


18.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Wizara imefanikiwa kukamilisha uandaaji wa Kanuni za Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 ambapo zilianza kutumika rasmi mwezi Novemba 2019. Aidha, Wizara imeanza kutekeleza Mpango Maalum wa Elimu kwa Umma kuhusu sekta hii ili kujenga uelewa kwa wananchi. Vile vile, Wizara imekamilisha kuandaa Mpango Kabambe wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha pamoja na Kanuni za Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Fedha. Ukurasa wa 16 -17 wa hotuba yangu unaainisha kwa kina kazi nyingine zilizofanyika katika kutekeleza jukumu hili muhimu kwa uchumi wetu kati ya Julai 2019 na Machi 2020.

(v)          Usimamizi wa Deni la Serikali


19.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Serikali ilifanikiwa kulipa deni lake lote lililoiva lenye thamani ya shilingi trilioni 6.19. Kati ya kiasi hicho, Deni la Ndani ni shilingi trilioni 4.06ikijumuisha riba shilingi trilioni 1.09na mtaji shilingi trilioni 2.98. Aidha, Deni la Nje ni shilingi trilioni 2.13ikijumuisha riba ya shilingi bilioni 636.75 na mtaji shilingi trilioni 1.49.

(vi)        Ubia kati ya Sekta ya umma na sekta binafsi


20.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Wizara imefanikisha kutungwa kwa Kanuni za Sheria ya Ubia za Mwaka 2020 na kutangazwa katika Gazeti la Serikali Na.37. Aidha, Wizara imeendelea kupokea, kuchambua na kutoa ushauri kwa Mamlaka za Serikali zinazotekeleza miradi ya PPP ipatayo 10 ambayo ipo katika hatua za awali za kutafuta wabia, washauri elekezi, kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina.

21.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Wizara inatarajia kukamilisha taratibu za kuanzisha kituo cha ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi - PPP Center.

(vii)      Usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma


22.      Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Msajili wa Hazina imeendelea kutekeleza jukumu lake la Usimamizi wa Taasisi na Mashirika ya Umma kama inavyooneka katika hotuba yangu ukurasa wa 23 -24. Aidha, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Mfuko Mkuu wa Serikali umepokea jumla ya shilingi bilioni 612.87 kutoka kwenye Taasisi na Mashirika ya Umma kama gawio na michango ya Mashirika.

(viii)    Taasisi za Mafunzo ya Elimu ya Juu na Bodi za Kitaaluma na Kitaalamu


23.      Mheshimiwa Spika, Wizara inasimamia Taasisi tano (5) za mafunzo ya elimu ya juu na Bodi mbili (2) za kitaaluma na kitaalamu ambazo ni: Chuo cha Usimamizi wa Fedha -IFM; Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini – IRDP; Taasisi ya Uhasibu Tanzania – TIA; Chuo cha Uhasibu Arusha –IAA; Chuo cha Takwimu Mashariki mwa Afrika – EASTC; Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi – PSPTB na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu – NBAA. Utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo na mpango wa utekelezaji kwa mwaka 2020/21 ni kama inavyoonekana katika kitabu cha hotuba yangu ukurasa wa 24 -27.

(ix)        Mafao ya Wastaafu na Mirathi


24.      Mheshimiwa Spika, kati ya mwezi Julai 2019 na Machi 2020, Wizara imelipa mafao na pensheni kwa wastaafu wa Serikali 57,605, mirathi kwa warithi 1,006 na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi 457 wa Serikali walio kwenye mikataba. Aidha, Wizara imeandaa vitambulisho vipya vya wastaafu vya kielektroniki katika mfumo wa “smart cards” na kuboresha Mfumo waunaotumika kutoa huduma kwa njia ya mtandao na kudhibiti fedha za mirathi zinazotoka HAZINA kwenda moja kwa moja kwenye akaunti za warithi (Tanzania Pensioners Payment System – TPPS).

(x)          Tume ya Pamoja ya Fedha


25.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2019/20, Tume ya Pamoja ya Fedha imefanya stadimaalum kuhusu Mfumo wa Biashara kati ya Tanzania Bara na Zanzibar na Mwenendo wa Mapato ya Muungano. Aidha, Tume imefanya uchambuzi wa taarifa na takwimu halisi za Mapato na Matumizi ya Muungano kwa mwaka 2017/18, mwaka 2018/19 na 2019/20. Taarifa ya uchambuzi wa takwimu hizo ilijadiliwa na Sekretarieti ya Tume mwezi Februari, 2020 na Serikali za pande zote zinaendelea kufanyia kazi mapendekezo yaliyomo katika taarifa hiyo.

(xi)        Sekta ya Michezo ya kubahatisha


26.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2020, Wizara imewezesha marekebisho ya  Sheria ya Michezo ya Kubahatisha SURA 41 ili kuipa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kudhibiti matangazo ya michezo ya kubahatisha. Aidha, Bodi inaendelea kuunda na kuunganisha mifumo ya TEHAMA ili kuimarisha udhibiti wa michezo ya kubahatisha.

(xii)       Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi


27.      Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha uwazi na uwajibikaji kwenye matumizi ya rasilimali za umma, hadi kufikia Machi 2020, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imefanya ukaguzi kwa mafungu 66 ya Wizara na Idara za Serikali; Wakala 33; Taasisi 48; Balozi 42; Vyama vya Siasa 19; Bodi za Mabonde ya Maji 14; Hospital za Rufaa 27, Mashirika ya Umma 150; Mamlaka za Serikali za Mitaa 185; Mikoa 26; na Mifuko Maalumu 16. Aidha, ofisi imefanikiwa kufanya ukaguzi wa usimamizi wa mikataba ya ujenzi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 19. Vile vile, ukaguzi umefanyika kwa miradi ya maendeleo 435 ikijumuisha miradi 65ya Serikali Kuu na miradi 370 ya Serikali za Mitaa.

28.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi imepanga kuimarisha ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo hadi ngazi za Tarafa, Kata na Vijiji; kufanya ukaguzi wa miradi mikubwa ya maendeleo (Reli ya Kisasa, Vivuko, Bomba la Gesi Mtwara na Ukarabati wa Reli ya Kati); kupanua mawanda ya ukaguzi katika eneo la uchimbaji wa madini, mafuta na gesi ikiwemo kuimarisha ukaguzi wa kiuchunguzi na kiufundi; na kuendelea kufanya ukaguzi wa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma pamoja na kufanya ukaguzi wa ufanisi.

Changamoto na Mikakati ya Kukabiliana nazo


Changamoto


29.      Mheshimiwa Spika,  utekelezaji wa majukumu ya Wizara  unakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo  tunaendelea kukabiliana nazo kwa kushirikiana na wadau wengine ili zisilete athari hasi katika malengo tuliyojiwekea. Baadhi ya changamoto hizo ni:

(i)     Kasi ndogo ya ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo katika Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa;
(ii)    Mabadiliko ya mara kwa mara ya teknolojia ya mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato yanayoleta uhitaji wa upatikanaji wa teknolojia mpya na kuboresha na kuhuisha teknolojia ya mifumo iliyopo ili kuongeza ufanisi;
(iii)  Kuongezeka kwa gharama za mikopo kwenye masoko ya fedha duniani kutokana na mabadiliko ya  sera za fedha katika nchi  zilizoendelea (hususan Marekani na Nchi za Ulaya);
(iv)  Uharibifu wa miundombinu ya barabara na madaraja kutokana na mafuriko; na
(v)    Mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19).


Mikakati ya Kukabiliana na Changamoto


30.      Mheshimiwa Spika, Baadhi ya hatua zinazochukuliwa na Wizara katika kukabiliana na changamoto za utekelezaji wa majukumu yake ni pamoja na:

(i)         Kuanza mchakato wa kutunga sera na mkakati wa ufuatiliaji na tathmini ya miradi na programu za maendeleo;
(ii)        Kujenga uwezo wa wataalam wa ndani katika kubuni, kuunda na kuhuisha teknolojia ya mifumo ya usimamizi na ukusanyaji wa mapato;
(iii)      Kuhamasisha wadau wa ndani kuendelea kushiriki katika minada ya dhamana za Serikali pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya mikopo ya nje vyenye riba nafuu; na
(iv)      Wizara imekamilisha uchambuzi wa taarifa mbalimbali za kisekta ili kubaini kiwango cha athari zitokanazo na  mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) katika uchumi na kuainisha mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu ya kukabiliana nazo. Taarifa jumuishi ya mikakati ya kupambana na CORONA imewasilishwa kwenye ngazi za maamuzi Serikalini.

3.0    MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA 2020/21

(i)        Makadirio ya Mapato

31.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Wizara inakadiria kukusanya maduhuli ya kiasi cha shilingi bilioni 973.02 kutoka katika vyanzo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na gawio, kodi za pango, marejesho ya mikopo, michango kutoka katika taasisi na mashirika ya umma, mauzo ya leseni za udalali na nyaraka za zabuni. Mchanganuo wa maduhuli yanayokadiriwa kukusanywa umeoneshwa katika kitabu cha hotuba ukurasa wa 34 katika Jedwali Na. 4.

(ii)              Makadirio ya Matumizi

32.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Wizara ya Fedha na Mipango inaomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi trilioni 12.39 kwa mafungu yotesaba (7) kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 11.73 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 659 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Kati ya matumizi ya kawaida, shilingi trilioni 10.48 kwa ajili ya deni la Serikali, shilingi bilioni 750.29 matumizi mengineyo na shilingi bilioni 510 kwa ajili ya mishahara na marekebisho ya mishahara. Aidha, matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi bilioni 624.7 fedha za ndani na shilingi bilioni 34.61 fedha za nje.

33.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2020/21, Fungu 45 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 80.5kwa ajili ya matumizi ya kawaida na ya maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 68.87 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 11.66 matumizi ya maendeleo. Matumizi ya kawaida yanajumuisha shilingi bilioni 14.88 kwa ajili ya mishahara na shilingi bilioni 53.99 matumizi mengineyo. Aidha, matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi bilioni 6.70 fedha za ndani na shilingi bilioni 4.96 fedha za nje. Mchanganuo wa kiasi kinachoombwa kwa kila fungu umeainishwa katika Jedwali Na. 5 lililopo katika hotuba yangu ukurasa wa 35.

     4.0  HITIMISHO

34.      Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kusema awali, Mkutano huu wa Bunge ni wa mwisho katika muhula huu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano. Napenda kutumia fursa hii kukiri kuwa, katika kipindi chote cha muhula huu, Wizara imenufaika sana na maoni na ushauri kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao umesaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha uchumi wa nchi yetu.

35.      Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine, naomba nirudie kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufanya kazi yake hii ya Waziri wa Fedha na Mipango aliyonipa kupitia Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, namshukuru tena Mheshimiwa Rais, kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii ngumu kwa miaka mitano mfululizo. Vilevile, napenda kuwashukuru wananchi wote wa Tanzania hususan kwa kufanya kazi na kulipa kodi ili kujenga uchumi wa nchi yetu. Nawaomba Watanzania tuendelee kuchapa kazi kama anavyotuasa Mheshimiwa Rais wetu na kuitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “HAPA KAZI TU”. 

36.      Mheshimiwa Spika, kutokana na janga la mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19), napenda kuchukua fursa hii kutoa pole kwa wananchi wote waliopatwa na madhara yanayotokana janga hili na kuwaasa kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huu kama inavyoelekezwa na wataalamu wa afya. Aidha, napenda kuwapongeza kwa dhati madaktari na watumishi wote wa Afya walio mstari wa mbele siku zote katika kutoa huduma kwa wananchi hasa wanyonge na hususan katika kipindi hiki cha mlipuko wa COVID-19 nchini. 

37.      Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa, napenda nikushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kuwasilisha hoja hii pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza. Aidha, nawashukuru wote walioshiriki katika maandalizi ya hotuba hii na kuhakikisha inakamilika kwa wakati. Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara kwa anuani ya www.mof.go.tz.

38.      Mheshimiwa Spika, naombakutoa hoja.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527