BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU YAANZA MAANDALIZI YA MALIPO KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU WANAOTEGEMEA KUFUNGUA JUNE 01


Tunapenda kuwajulisha wanafunzi wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kupitia HESLB kuwa, tumeanza kufanya malipo yenye jumla ya thamani ya TZS 63.7 bilioni ikiwa ni fedha za chakula na malazi kwa ajili ya robo ya tatu ya mwaka wa masomo 2019/2020 na fedha hizo zitawafikia wanufaika wote kupitia vyuo vyao ifikapo Alhamisi, Mei 28, 2020.

Hatua hii ya kuanza kufanya malipo inafuatia maelekezo ya kufunguliwa kwa taasisi za elimu ya juu ifikapo Juni 1, 2020 ambayo yametolewa  (Alhamisi, Mei 21, 2020) na Mheshimiwa  Rais, Dkt. John Magufuli jijini Dodoma. Serikali ilifunga shule na vyuo Machi 16, 2020 kama sehemu ya jitihada za kupambana na maambukizo ya virusi vya corona na ugonjwa wa COVID-19.

Kwa utaratibu uliopo, fedha za chakula na malazi hulipwa kwa mwanafunzi mnufaika mara nne katika kila mwaka wa masomo, yaani kila baada ya siku 60 za masomo ambazo mwanafunzi anapaswa kuwepo chuoni.

“Hadi wakati vyuo vinafungwa, wanafunzi wanufaika walikuwa wameshalipwa malipo ya robo ya kwanza ambayo yalilipwa Novemba, 2019 na robo ya pili yaliyolipwa mwezi Januari, 2020,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru leo (Alhamisi, Mei 21, 2020) jijini Dar es salaam.

Wakati huohuo, pamoja na malipo ya fedha za chakula na malazi kwa wanafunzi, HESLB pia inakamilisha malipo yenye thamani ya TZS 59.1 bilioni ya ada za wanafunzi wanufaika ambayo yatalipwa kwa taasisi zaidi ya 70 za elimu ya juu zilizopo nchini.

Malipo ya ada hulipwa vyuoni mara mbili kwa mwaka, yaani mwanzoni mwa muhula wa mwaka wa masomo mara baada ya HESLB kupokea uthibitisho wa usajili wa wanafunzi vyuoni na mwanzoni mwa muhula wa pili, mwezi Machi.

"Lengo la malipo haya ni kuziwezesha taasisi za elimu kumudu gharama za uendeshaji na hivyo kutoa elimu inayokusudiwa kwa wanafunzi wanaosoma katika taasisi zao,” amesema Badru leo (Alhamisi, Mei 21, 2020) jijini Dar es salaam na kuongeza kuwa malipo ya ada yatakuwa yamevikia vyuo vyote vilivyowasilisha hati za madai HESLB ifikapo Ijumaa, Mei 29, 2020.

Katika mwaka wa masomo 2019/2020, Serikali inatoa mikopo ya elimu ya juu yenye jumla ya thamani ya TZS 450 bilioni kwa wanufaika 132,119 wanasoma katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu hapa nchini. Fedha hizi zinagharamia vipengele sita ambavyo ni chakula na malazi; ada; vitabu na viandikwa; utafiti; mafunzo kwa vitendo; na mahitaji maalum kwa baadhi ya vitivo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post