BASI LA PREMIER LAPATA AJALI USANDA SHINYANGA..59 WANUSURIKA KIFO,WAMO WANAFUNZI WA VYUOWatu 59 waliokuwa wakisafiri kutoka Jijini Mwanza kwenda Mbeya wamenusurika na kifo mara baada ya basi walilokuwa wakisafiria Premier lenye namba za usajili T, 629 AET, linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Mbeya kupata ajali katika kijiji cha Ngaganulwa Usanda wilayani Shinyanga na kusababisha majeruhi Saba.Akisimulia, mashuhuda wa ajali hiyo Robart Samwel aMEsema tukio hilo limetokea leo Ijumaa Mei 29,2020 majira ya saa 3 asubuhi katika eneo hilo, ambapo kulikuwa na mabasi mawili yamesimama ndipo basi hilo likiwa katika mwendokasi lilishindwa kusimama na hatimaye dereva kulikwepesha na kuanguka.

Alisema katika eneo hilo kulikuwa na basi la Abood limesimama upande wa kushoto na jingine la Ally's Bus upande wa kulia, ambapo basi hilo la Premier lilianza kufunga breki na baada ya dereva kuona limemshinda ndipo akalikwepesha vichakani na kuanguka chini.

“Nimeishuhudia ajali ya basi hili la Premier kwa macho yangu kabisa, ambapo pembeni ya barabara kulikuwa na basi la Abood limesimama na upande mwingine kulikuwa na basi la Allys, ndipo basi hili likiwa katika mwendo kasi lilishindwa kusimama na kusababisha ajali,” alisema Samweli.

Nao baadhi ya abiria akiwemo Justice Alyoce ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha Sita ,alisema wakati akitokea jijini Mwanza basi hilo la Premier pamoja na Abood yalikuwa yakifukuzana ndipo walipofika eneo hilo na kukuta mabasi la Abood na Allys yamesimama likamshinda ndipo ikatokea ajali.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga ACP Debora Magiligimba ambaye alikuwa eneo la tukio, alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi, ambapo dereva wa basi la Premier alipofika eneo hilo na kukuta mabasi mawili yamesimama pande zote basi lilimshinda na hatimaye kuanguka.

Aidha alisema basi hilo lilikuwa limebeba abiria 59 wakiwamo wanafunzi, huku akiwataja majeruhi saba wa ajali hiyo kuwa ni Thabiti Abdul, Swaumu Kisandu, Mohamed Nyerere, Betha Minami, Mohamed Ahmed, Ilham Yahya, pamoja na Haida Hassani.

Alisema majeruhi hao wote wamepata majeraha katika maeneo mbalimbali ya viungo vyao vya miili yao, ambapo walikimbizwa kupatiwa matibabu katika kituo cha afya Tinde kilichopo karibu na eneo la ajali,na kwamba hakuna kifo, na kubainisha wanamtafuta dereva wa basi hilo ambaye amekimbia kusikojulikana.


TAZAMA PICHA HAPA CHINIBasi la Premier lenye namba za usajili T, 629 AET linalofanya safari zake kutoka Mwanza kwenda Mbeya likiwa limepata ajali katika eneo la Ngaganulwa- Usanda wilayani Shinyanga na kusababisha majeruhi saba. Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga  ACP Debora Magiligimba akiwa eneo la tukio na kuzungumzia chanzo cha ajali hiyo.

Abiria Justice Aloyce ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha Sita Jijijni Mbeya akielezea namna ajali ilivyoanza kutokea sababu ya uzembe wa dereva. kutokea Jijini Mwanza.

Muonekano wa basi la Premier likiwa limeanguka chini mara baada ya kupata ajali.

Picha zote na Marco Maduhu - Malunde 1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527