AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KUIBA PIKIPIKI YA BOSI WAKE MJINI KAHAMA

Na Salvatory Ntandu - Kahama

Mkazi wa mtaa wa Muhongolo Aron Salvatory Chubwa amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Kahama kwa tuhuma ya wizi wa kuiba pikipiki ya mwajiri wake yenye thamani ya shilingi milioni tatu.


Mbele ya Hakimu mkazi wa Mahakama hiyo leo Aprili 27,2020 Christina Laurent Chovenye,Mwendesha Mashitaka wa Jeshi la Polisi Athumani Kisango alidai kuwa Salvatory alitenda kosa hilo Aprili 8 mwaka huu katika eneo la Cool breezy Mjini Kahama.

Alisema kuwa Mtuhumiwa katika shauri hilo la jinai namba 133 la mwaka huu alitenda kosa hilo la wizi wa kuaminiwa kinyume na kifungu mamba 258 (1)273(b) sura ya 16 ya kanuni ya adhabu marejeo ya mwaka 2019.

"Aron aliiba piki piki ya mwajiri wake Omary Musa yenye namba za usajili MC 747 CSC baada ya kuikabidhiwa kwa ajili ya kufanya kazi ya kusafirisha abiria katika maeneo mbalimbali mjini humo,"alisema Kisango.

Hata hivyo Aron amekana shitaka hilo na limeahirishwa hadi Mei 11 mwaka huu na amerudishwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post