WAANDISHI WA HABARI WAANDIKE HABARI ZENYE MSAADA KWA JAMII KIPINDI HIKI CHA COVID - 19


Waandishi wa habari wakiendelea na majukumu yao mkoani Shinyanga

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Vyombo vya Habari ni moja ya sehemu ambayo inatoa tarifa kwa wananchi na kujua hali ya nchi inavyoendelea katika kipindi husika.

Kazi ya Vyombo vya habari inalindwa na Katiba ya nchi ya mwaka 1977,ibara ya 18 kifungu a hadi d ambapo vinaeleza bila kuathiri sheria ya nchi,kila mtu yupo huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake na kutafuta ama kupokea na kutoa habari kupitia chombo chochote cha habari.

Pia ibara hiyo inaeleza kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali yanayoendelea nchini na duniani ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi.

Rose Reuben ni Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA),anaelezea umuhimu wa habari kwa wananchi kipindi hiki cha COVID-19.

Anasema wanahabari wanapaswa kuhakikisha wanaendelea kutoa taarifa kwa wingi zaidi na zenye kujibu maswali ya wananchi hususani katika kipindi hiki cha Mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19(corona)

Anasema ni wajibu wa wanahabari kuhabarisha wananchi juu ya mwenendo wa ugonjwa huu kwa kutoa habari zilizo sahihi ambazo zitawatoa hofu wananchi na kuwaelimisha namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Anasema kwa kipindi hiki wanahabari wanapaswa kusaidia serikali katika kufikisha taarifa sahihi kwa wanajamii na kusaidia wanajamii kuchukua tahadhari.

"Ni nafasi ya wanahabari kuandika kutoa na kuandika habari za uhakika ambazo zinakuwa msaada katika jamii hususani katika kipindi hiki watu wanataka kujua umuhimu wa uvaaji wa barakoa wengine kujua namna ya kujinga wasiweze kupata maambukizi ya ugonjwa huu ni muhimu sana kutoa taarifa hizi,”anasema Rubern

Anasema Waandishi wa habari ni daraja kati ya Jamii na Serikali katika kujibu majibu yao hivyo ni jambo jema la kupokea taarifa zilizosahihi.

Kwa Upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Kajubi Mkajanga anasema baraza limekuwa likisisitiza majukumu na uwajibikaji upo pande mbili kwa watoa habari ,Mamlaka husika na waandishi wa habari .

Anasema kwa kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID-19 wamekuwa wakiwahimiza waandishi wa habari kuzingatia muongozo uliotolewa na Baraza hilo katika kufanya kazi kipindi hiki.

Kajubi anasema uhuru wa Kuandika habari nikuhakikisha waandishi wa habari wanaandika habari kwa usahihi kufata vigezo na misingi ,taaluma na Maadili ya uandishi wa habari katika kuwafikishia wananchi habari.

“Kwa upande wa watoa taarifa Watanzania wana haki ya kupata taarifa juu ya ugonjwa huu,taarifa zilizosahihi na kuzipata kwa haraka sio wakati wa kuonyeshana umashuhuri ni vema habari zikatolewa kwa uhakika na zisicheleweshwe,’’anasema.

Anasema wanaomba vyombo vya mamlaka kutokimbilia kutoa adhabu kwa vyombo vya habari kipindi hiki bali kiwe kipindi cha kuelimishana kutokana na kipindi hiki cha Covid-19 kuwa kipya.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post