Tanzia : MWANAHARAKATI WA KUTETEA HAKI ZA WATU WENYE UALBINO JOSEPHAT TORNER AFARIKI DUNIA KWA AJALI YA GARI


Josephat Torner enzi za uhai wake

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Mkurugenzi wa Idara ya Ushawishi na Utetezi wa Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na Utetezi wa haki za Watu wenye Ualbino iitwayo Foundation of Josephat Torner Europe Aid (FOJOTEA) ambaye amewahi kuwa Afisa Mahusiano na Habari wa Chama cha watu wenye Ualbino nchini Tanzania (TAS), Josephat Torner Nkwabi (42) amefariki dunia baada ya kugongwa na Hiace ‘ Daladala’ akivuka barabara jijini Mwanza.


Akizungumza na Malunde 1 blog, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema Josephat Torner amefariki dunia jana Aprili 12,2020 majira ya saa mbili usiku baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili T263 CZQ Toyota Hiace Daladala katika Barabara ya Makongoro jijini Mwanza. 



“Josephat Torner mkazi wa Gana Mwanza ambye ni mtu mwenye ualbino aligongwa na Daladala na kufariki dunia katika barabara ya Makongoro eneo la Kifua wazi karibu na Rock City Mall kata ya Kirumba iliyoendeshwa Emmanuel Mwanasalaha”,amesema Kamanda Muliro. 



“Daladala hiyo iliyokuwa inatokea Mjini kwenda Nyasaka ilimgonga Josephat Torner ambaye alikuwa akivuka barabara kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine",amesema Kamanda Muliro.



Kamanda Muliro amesema dereva wa gari hiyo alikimbia na kutelekeza gari na Jeshi la polisi linamshikilia mmiliki wa gari hiyo huku juhudi za kumtafuta dereva wa gari zikiendelea.

Soma Pia : WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA WAMLILIA JOSEPHAT TORNER


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post