WAANDISHI WA HABARI SHINYANGA WAMLILIA JOSEPHAT TORNER

Josephat Torner enzi za uhai wake


SALAMU ZA POLE NA RAMBIRAMBI MSIBA WA JOSEPHAT TORNER

Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC) kimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mdau wa haki za watu wenye ualbino Josephat Torner Nkwabi  (42) ambaye amefariki dunia Aprili 12,2020 kwa ajali ya  gari /kugongwa na Hiace ‘Daladala’ akivuka barabara jijini Mwanza.

Josephat Torner atakumbukwa kwa ushirikiano wake mkubwa SPC na waandishi wa habari kwa ujumla katika kutetea na kulinda haki za watu wenye Ualbino mkoani Shinyanga na maeneo mbalimbali nchini hususani mikoa ya Kanda ya Ziwa ambayo ilikuwa inasifika kwa mauaji ya watu wenye ualbino.

SPC imeshiriana na Josephat Torner kutetea haki za Watu wenye Ualbino tangu akiwa Afisa Mahusiano na Habari wa Chama cha watu wenye Ualbino nchini Tanzania (TAS) na hata alipoanzisha Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na Utetezi wa haki za Watu wenye Ualbino iitwayo Foundation of Josephat Torner Europe Aid (FOJOTEA) awali ikijulikana Josephat Torner Foundation Europe (JTFE) akiwa Mkurugenzi wa Idara ya Ushawishi na Utetezi wa taasisi hiyo akitumia Kauli mbiu ya “Vunja Ukimya,Linda watu wenye ualbino”.

Kupitia taarifa hii Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga kinatuma salamu za pole za rambirambi kwa Chama Cha Watu Wenye Ualbino Tanzania (Tanzania Albinism Society – TAS), Familia ya Josephat Torner na FOTOJOA kwa kumpoteza ndugu Josephat Torner.

Tukiwa wadau wa kutetea haki za Watu Wenye Ualbino,tunasikitika kwa pamoja na ndugu,jamaa na marafiki kufuatia msiba huu mzito.

Bwana alitoa,Bwana ametwaa,Jina la Bwana Lihimidiwe

Imetolewa leo Jumatatu Aprili 13,2020 na:
Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club -SPC)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post